Naibu Waziri wa Afya Harous Said Suleiman akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Uzinduzi wa Zoezi la Utoaji wa Matone ya Vitamin A na Dawa za Minyoo kwa Watoto litakaloanza tarehe 5/12/2019 katika vituo vyote vya Afya Unguja na Pemba hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Wizara hio Mnazi mmoja Zanzibar.
Mkuu wa kitengo cha lishe Zanzibar Asha Hassan Suleiman akijibu maswali yalioulizwa na Waandishi wa Habari katika Mkutano wa Naibu Waziri wa Afya kuhusiana na Uzinduzi wa Zoezi la Utoaji wa Matone ya Vitamin A na Dawa za Minyoo kwa Watoto litakaloanza tarehe 5/12/2019 katika vituo vyote vya Afya Unguja na Pemba hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Wizara hio Mnazi mmoja Zanzibar.
…………………
Khadija Khamis- Maelezo Zanzibar
Wizara ya Afya Zanzibar imewataka viongozi wa ngazi za wilaya kisiasa na kidini kuwahamasisha wananchi kushiriki katika kampeni ya chanjo ya Matone ya Vitamin ‘A’ na minyoo inayotarajia kutolewa tarehe 5 hadi 31 mwezi huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Naibu Waziri wa Wizara hiyo Harusi Saidi Suleiman amesema utowaji wa matone hayo utafanyika katika vituo vyote vya afya pamoja na vituo maalum kwa siku ya Jumamosi na Jumapili.
Amesema katika kampeni hiyo zaidi ya watoto wenye umri wa miezi sita watapatiwa chanjo ya Vitamin ‘A’ na upimaji wa hali ya lishe na umri wa mwaka mmoja hadi mitano watapatiwa matone ya Vitamin ‘A’ na dawa za minyoo
Amesema lengo la serikali kuwahamasisha wananchi kutambua umuhimu wa kuwapeleka watoto wao vituo vya afya kwa kuwapatia chanjo hizo ili waweze kukua wakiwa na afya bora kuepukana na utapiamlo
“Wananchi mshiriki katika kampeni hii kwa kuwapeleka watoto wanu kupatiwa chanjo hiyo na dawa za minyoo ili kuokoa maisha yao na kukuwa katika afya njema,”alisema Naibu Waziri .
Nae Mkuu wa kitengo cha lishe Asha Hassan salmini amewataka wazazi na walezi kuvitumia vyakula vya asili vikiwemo matunda na mboga mboga kwa watoto wa umri ya chini ya miaka mitano kwa ajili ya kufikia mahitaji yao ya kupatiwa virutubisho vya nyongeza .
Aidha alisema kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwa mpangilio kutasaidia ongezeko la vitamin mwilini mwao kwani maziwa ya mama yana vitamin vya aina zote
Kampeni ya chanjo ya matone ya Vitamin ‘A’ na dawa za minyoo hutolewa mwaka mara mbili ambapo mwaka huu zilianza Mwezi June na Kumalizia Disembar .