Viongozi wa Mkoa wa Tabora na Wilaya ya Kaliua wakiwa nje ya jengo la Makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Kaliua wakati wa ziara yao ya kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi huo unaoendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (katikati) akitoa maelekezo kwa Watendaji na viongozi mbalimbali mara baada ya kukagua maendeleleo ya ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Kaliua jana.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (kulia) akipima urefu wa kuta mbalimbali wakati wa ukaguzi wa maendeleleo ya ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Kaliua jana.
………………..
NA TIGANYA VINCENT
MKUU wa Mkoa wa Tabora aggrey Mwanri amemwagiza Mhandisi wa ujenzi wa Ofisi yake kuchunguza vipimo vya nyumba ya makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Kaliua ili kujiridhisha kama Mkandarasi amefuata maelekezo yaliyopo kwenye ramani ya ujenzi.
Alichukua hatua hiyo baada ya kubaini sehemu ya ukuta wa sebule katika nyumba hiyo kurudishwa ndani mita moja na kuwa sita badala ya saba ambazo ndio zinaoonyeshwa kwenye mchoro wa ramani ya ujenzi.
Mkuu wa Mkoa alitoa agizo hilo jana Wilayani Kaliua wakati alipoongoza Kamati ya Mkoa wa Tabora ya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa baada ya kupata fedha toka Serikalini.
Alisema kama itabainika kuwa Mkandarasi amesogeza ndani ukuta kwa ajili ya kupunguza vipimo itabidi akatwe sehemu ya fedha zake ili kufidia sehemu ambayo imepunguzwa.
“Kwa sababu jengo limeshafika hatua ya uezekaji , hatuwezi kumwambia abomoe lakini tunachotaka kujua vipimo vya upana na urefu wa vyumba kama viko sawa na kama haviko sawa kulingana na mchoro tumkate fedha” alisema.
Nyumba hiyo ya makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Kaliua inaendelea kujengwa na Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) inatarajia kutumia shilingi milioni 199.6 hadi itakapokamilika.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alimwagiza Mkandarasi huyo kuhakikisha anafanyia marekebisho eneo la ndani ya Choo katika nyumba ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaliua kabla ya kuikabidhi kwa uongozi wa Wilaya ili kuondoa mapungufu yaliyoonekana.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu alisema kuwa mchakato wa awali wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kaliua umeanza na tayari wameshapokea shilingi milioni 350 kwa ajili ya kuanza kazi za awali za ujenzi wa Ofisi hiyo ambapo tayari uchunguzi udongo umeshafanyika.
Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa alisema kuwa awali walitaka kutumia Shirika la Nyumba la Taifa katika ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya lakini wakadai shilingi bilioni 1.400 ikiwa ni gharama za ujenzi pekee tu bila kuweka gharama za ununuzi wa vifaa.
Alisema hatua hiyo iliwafanya kuachana nao na kuendelea kutafuta Wakandarasi wengine ambao watajenga jengo hilo kwa ubora unaotakiwa kwa gharama za chini.