Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani (Wa kwanza kulia) akipatiwa maelezo kuhusu usindikaji katika kiwanda cha maziwa cha Chama cha Ushirika wa Maziwa wa Wanawake Nronga kutoka kwa Katibu Meneja wa chama hicho, Hellen Usiri.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani (Wa kwanza kulia) akinywa maziwa yanayosindikwa na kiwanda cha Chama cha Ushirika wa Maziwa wa Wanawake Nronga, kwenye ATM ya Maziwa ya Nronga Youth Service Group.
Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kilimanjaro, John Henjewele akiongea kwenye ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani kwenye kiwanda kusindika maziwa cha Chama cha Ushirika wa Maziwa wa Wanawake Nronga.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani (Mwenye tai) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa kiwanda cha kusindika maziwa cha Chama cha Ushirika wa wa Wanawake Nronga.
………………
Moshi,
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani amewataka Wafugaji kote nchini kujiunga pamoja katika Vyama vya Ushirika ili kuwa na nguvu ya pamoja na kuweza kuyaaongezea thamani mazao ya mifugo ikiwemo kuanzisha Vyama vya Ushirika wa Maziwa.
Dkt. Kamani ametoa wito huo leo Jumatatu, Desemba 2, 2019 kwenye ziara ya kutembelea na kujionea mafanikio na changamoto za Chama cha Ushirika wa Maziwa wa Wanawake Nronga (Nronga Women Dairy Cooperative Society) kilichopo wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
“kutokana na nilichojionea hapa kwenye kiwanda cha kusindika maziwa cha Chama cha Ushirika wa Maziwa wa Wanawake Nronga, na kwa kuwa nchi hii ina utajiri mwingi wa ng’ombe wa asili na kisasa, nawasihi wafugaji wajiunge pamoja katika ushirika na kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa vya kusindika maziwa na bidhaa zake na kuwanufaisha wananchi wengi Zaidi kwa kuwapatia ajira na kuwaongezea kipato,” amesema Dkt. Kamani.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania amesema kuwa mfano uliooneshwa na wanawake wa Nronga hauna budi kuigwa na wafugaji katika mikoa inayosifika kwa kuwa na mifugo mingi ili waweze kujiunga pamoja katika ushirika na kuweza kupata manufaa makubwa kutokana na kusindika maziwa na kujipatia bidhaa nyingine zinazotokana na maziwa.
“Ni vigumu mfugaji mmoja mmoja kuweza kuanzisha kiwanda cha kusindika maziwa, lakini wafugaji wakijiunga katika ushirika wataweza kukusanya maziwa yao kwa pamoja na kutafuta mashine zitakazowawezesha kufanya usindindikaji na kukuza mataji na hatimaye kuweza kumiliki kiwanda chao wenyewe,” amesema Dkt. Kamani.
Akitoa maelezo kuhusu Chama cha Ushirika wa Maziwa wa Wanawake Nronga kwa Dkt. Kamani, Katibu Meneja wa chama hicho, Hellen Usiri amesema kuwa chama chake kilianzishwa na wanawake 6 mwaka 1987 na hivi sasa kina wanachama 462.
Tangu Nronga Women Dairy Cooperative Society ianzishwe imeweza kupata mafanikio mbalimbali kwa jamii ndani na nje ya Nronga ikiwemo: ongezeko la kipato kwa kaya, kusomesha Watoto, kuboresha mifugo ya wanachama, kuboresha makazi (nyumba bora), wanachama kufungiwa mitambo ya biogas na kutengeneza mbolea hai itokanayo na mbolea itokayo kwenye mitambo ya biogas.
Mafanikio mengine ya Chama cha Ushirika wa Maziwa wa Wanawake Nronga ni pamoja na Kutekeleza Mradi wa unywaji maziwa shuleni kwa baadhi ya shule za msingi zilizopo katika wilaya ya Hai, Kuanzisha SACCOS, kutoa mafunzo kwa vyama na vikundi vya maziwa ndani na nje ya Nronga na kuongoza jitihada za uanzishwaji wa Joint Enterprise (JE) kwa vikundivilivyokowilaya ya Hai vinavyojishughulisha na ukusanyaji na usindikajiwa maziwa.
Aidha, Chama cha Ushirika wa Maziwa wa Wanawake Nronga kimefanikiwa kuanzisha kiwanda cha maziwa na kimeweza kutengeneza bidhaa mbalimbali na bora zinazotokana na maziwa kama vile mtindi, yogati pamoja na siagi.