Home Mchanganyiko SHIRIKA LA MEDO LAGUSWA WANAFUNZI WASIONA KUSOMEA NJE MKOANI SINGIDA

SHIRIKA LA MEDO LAGUSWA WANAFUNZI WASIONA KUSOMEA NJE MKOANI SINGIDA

0
  Mwalimu Hemed Kilango akiwafundisha Wanafunzi  wenye ulemavu wa kuona na uoni hafifu wa  Shule ya Msingi Mgori iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida jana ambao usomea nje kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa.

 Mratibu wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Mtinko Education Development Organization (MEDO),  Idd Hashim, akizungumza na wadau wa elimu, walimu na wanafunzi wa shule hiyo katika kikao kujadili changamoto mbalimbali walizonazo wanafunzi hao.

 Afisa Elimu Maalumu Wilaya ya Singida, Huruma Fundah, akizungumza katika kikao hicho cha wadau.
Viongozi wa Kata  ya Migori wakijadiliana. Kutoka kushoto ni Diwani, Selemani Abdallah, Mwenyekiti wa Shule hiyo, Esther Isack, Afisa Mtendaji Leonard Muna na Afisa Maendeleo ya Jamii, Judith Cosaggy.
 
Na Waandishi wetu Singida 
 
SHIRIKA lisilokuwa la Kiserikali la Mtinko Education Development Organization (MEDO)  limeguswa na changamoto ya Wanafunzi  wenye ulemavu wa kuona na uoni hafifu katika Shule ya Msingi Mgori iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida  kusomea nje kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa. 
 
Wakitembelea shule hiyo yenye wanafunzi mchanganyiko jana,  wadau wa elimu wakiongozwa na maofisa wa shirika hilo walisikitishwa na jambo hilo na kusema kuwa hali hiyo inaashiria kuwepo kwa ubaguzi dhidi ya kundi hilo.
 
Shule hiyo ina kituo  kinacho hudumia wanafunzi hao wenye ulemavu wa uoni katika halmashauri  nzima ya Singida lakini miundombinu yake si rafiki kwa watoto hao kutokana na kutokuwa na sehemu nzuri ya kujifunzia hivyo wadau hao wanaiomba serikali kuwajengea darasa.
 
Mratibu wa shirika hilo,  Idd Hashim aliwaomba wadau na jamii kwa ujumla kuendelea kuwakumbusha viongozi ili kutatua changamoto hizo zinazowakabili walemavu hao, kwani ndio wajibu wao na mwisho wa siku waweze kupata huduma zilizo bora.
 
Hata hivyo wadau wamelipongeza shirika hilo kwa kuibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wenye uhitaji maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ili serikali iweze kuzitatua, na kuiomba serikali kuongeza vyuo vya walimu wa vitengo maalum ili kuondoa upungufu wa walimu hao ambalo ni janga kwa nchi nzima.