Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akiangalia hanadaki lililotumiwa na Samora Mashel lililopo wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati akitembelea maeneo ya historia ya Ukombozi wa Afrika.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akiwa ndani ya hanadaki lililotumiwa na Samora Mashel lililopo wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati akitembelea maeneo ya historia ya Ukombozi wa Afrika.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akiongea na Mama Loisa Kamwaya (aliyevaa kilemba) akiwa miongoni mwa Watanzania walioolewa na Wanamimbia waliokaa Wilaya ya Kongwa mkoa wa Dodoma wakati wa kupingania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Deogratius Ndejembi.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akimsikiliza Mama Loisa Kamwaya (aliyevaa kilemba) akiwa miongoni mwa Watanzania walioolewa na Wanamimbia waliokaa Wilaya ya Kongwa mkoa wa Dodoma wakati wa kupingania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Deogratius Ndejembi (aliyevaa kaunda) akiongea na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza (wa pili kulia) wakati akitembelea maeneo ya historia ya Ukombozi wa Afrika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
…………………
Na Eleuteri Mangi, Kongwa
Serikali inaendelea kubainisha maeneo yaliyotumiwa na wapingania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika ambayo yanasimamiwa kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika iliyopo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Akiwa katika ziara ya kikazi wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati akitembelea maeneo ya historia ya Ukombozi wa Afrika, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema kuwa Serikali kupitia wizara hiyo inaandaa sheria ya kulinda na kuhifadhi urithi wa ukombozi wa Afrika unaopatikana nchini.
“Lengo kubwa ni kuhakikisha maeneo haya yanalindwa kisheria ili yaweze kutumika kama vivutio vya utalii wa kiutamaduni pamoja na utalii wa kihistoria kwa sababu huu ni urithi muhimu wa historia nzuri ya nchi yetu, haya ni maeneo yaliyotumika kusaidia ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika” alisema Naibu Waziri Shonza.
Katika kutekeleza Programu ya Uhifadhi na Uendelezaji wa historia ya Ukombozi wa Afrika, Wizara inaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo, ukarabati wa jengo lililokuwa la Kamati ya Ukombozi ya iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambayo kwa sasa ni Umoja wa Afrika (AU).
Kazi nyingine ambazo Serikali imekamilisha ni uandaaji wa tovuti ya Programu, ubainishaji wa maeneo yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi, utambuzi wa nyaraka na vitu mbalimbali vinavyohusiana na harakati hizo pamoja na kufanya mahojiano na watu walioshiriki au kushuhudia harakati za ukombozi wa Afrika ambayo yamehifadhiwa kwa njia ya kidigitali.
Mji wa Kongwa kihistoria ni kitovu cha harakati za Ukombozi wa Afrika kwani harakati zote za mapambano ya kutafuta uhuru zilianzia Kongwa na baadaye zikaendelea katika maeneo mengine nchini kama sehemu ya kupanua wigo wa harakati hizo na huduma kwa Wapigania Uhuru.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Deogratius Ndejembi amesema kuwa Kongwa ni eneo kongwe lililotumiwa na Wapigania uhuru kutoka vyama mbalimbali vya Ukombozi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa eneo hilo lilitumika kwa ajili ya mafunzo kwa wapigania uhuru ambapo kwa sasa lina vielelezo muhimu vya kihistoria vilivyopo katika eneo hilo yakiwemo maeneo ya Handaki alilokuwa akilitumia Samora Mashel, nyumba za Makazi kwa wapigania uhuru, majengo ya shule ya sekondari Kongwa, eneo la Mafunzo ya kijeshi, kiwanja cha ndege na makaburi ya wapigania uhuru.
Maeneo mengine ya kihistoria ni makaburi ya mashujaa wa harakati za ukombozi ambayo jumla yake ni 11; makaburi matano ya wapigania uhuru kutoka Msumbiji, makaburi matatu ya wapigania uhuru kutoka Afrika Kusini na makaburi matatu ya wapigania uhuru kutoka Namibia.
Naibu Waziri Shonza yupo katika ziara ya kikazi kutembelea maeneo ya ya historia ya ukombozi wa Afrika katika mikoa ya Dodoma wilaya ya Kongwa, Morogoro wilaya Kilosa, Manispaa ya Morogoro pamoja na Mkoa wa Pwani wilaya za Chalinze na Bagamoyo.