Baadhi ya wakazi wa Igunga mjini wakiwa wamejipanga mstari kwa ajili ya kuchunguza afya zao ikiwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani juzi ambapo kwa Mkoa wa Tabora imefanyika Igunga .
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu (kulia) akiongozana juzi na Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo kwenda katika ukaguzi wa mabanda ya utoaji wa huduma za afya mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Rutatinisibwa akitoa maelezo mafupi juzi kuhusu hali ya maambukizi ya UKIMWI Mkoani humo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku yaUKIMWI Duniani.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo akitoa salamu za Wilaya wakati wa maadhimisho ya UKIMWI juzi ambapo yalifanyika Kimkoa wilayani humo.
………………….
NA TIGANYA VINCENT
WASICHANA Mkoani Tabora wametakiwa kuwa na ujasiri wa kusema hapana pindi wanaposhaushiwa na wanaume kupokea zawadi kwa lengo la kuwataka wajiingize katika vitendo vya kujamiana ambavyo vinawaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vinavyosababisha UKIMWI.
Kauli hiyo imetolewa juzi wilayani Igunga na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu wakati wa maadhimisho ya UKIMWI Duniani ambapo kimkoa yalifanyika wilayani humo ambapo kauli mbiu ilikuwa Jamii ni chachu ya mabadiliko , tuungane kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI.
Alisema wanapochukua zawadi zenye hila na kupakizwa katika vyombo mbalimbali vya usafiri wanakuwa wamejiingiza katika mtego wa kudaiwa jambo ambalo litawaingiza katika vitendo vinavyo hatarisha maisha yao.
“Ukizoea kupokea zawadi na kupewa ‘rift’ za magari na pikipiki , ipo siku na wewe utaombwa ‘rift’ ndipo kitakuwa chanzo cha kujiweka katika hatari na kupata maambuzi ya UKIMWI na wakati mwingine kupoteza ndoto yako ya kupata elimu” alisisitiza.
Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliitaka jamii kuendelea kuzingatia ushauri na elimu wanayopata ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa ajili ya kujikinga wao na familia zao na kuwa na jamii yenye afya njema.
Alisema maambukizi ya VVU yamekuwa na athari kubwa ya kiuchumi na hata watoto wengine wanalazimika kuacha masomo kwa ajili ya kuwahudumia wazazi wao na wengine kujiingiza katika utumikishwaji kwa sababu ya kutafuta fedha za kuwasaidia wadogo wao waliachwa na wazazi.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo alisema katika kukabiliana na kuenea kwa maambukizi mapya miongoni mwa Wanafunzi wa Shule za Sekondari wilayani humo amepiga marufuku sherehe za wanafunzi ambazo sio rasmi ambazo zinawachochea kufanya vitendo viovu.
Alisema kumezuka utaratibu ambao ni hatari kwa baadhi ya wanafunzi wanaohitimu Kidato cha Nne na Sita kuchangishana fedha na kukodi kumbi na vyumba kwa ajili kuwafanya sherehe ambayo hata walimu na wazazi hawana taarifa.
Mwaipopo alisema katika sherehe hiyo ambayo sio rasmi kuna vitendo hatari vinafanyika humo ambavyo vinaweza kuwasababisha kupata maambukizi ya VVU.