Mdau wa Maendeleo wa Kata ya Mitundu katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Mhandisi Felix Dagaki (katikati) akizungumza wakati akiongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti wa Jangwani uliopo katika kata hiyo mwishoni mwa wiki.
Imam wa msikiti huo, Salehe Faida (kulia) akimkabidhi risala mgeni rasmi, Mhandisi Felix Dagaki
Mwalimu wa madrasa katika msikiti huo, Hussein Omari (kulia) akipokea fedha zilizopatikana katika harambee hiyo. Kushoto ni Imam wa Msikiti Mkuu wa Kata ya Mitundu, Mohammed Issa.
Mdau wa Maendeleo wa Kata ya Mitundu katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Mhandisi Felix Dagaki (wa tatu kulia), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa dini ya kiislam. Kutoka kushoto ni Imam wa Msikiti Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Nawawi, Sheikh wa Kata ya Mitundu, Abdillahi Hassan, Sheikh Msaidizi wa Msikiti Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Sheikh Jamal na Mwalimu wa Dini Msikiti Mkuu wa Mitundu, Dkt. Salehe Pazzy.
Na Mwandishi Wetu, Singida
MDAU wa Maendeleo wa Kata ya Mitundu katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida, Mhandisi Felix Dagaki ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti wa Jangwani uliopo katika kata hiyo.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Mhandisi Dagaki, Imam wa msikiti huo, Salehe Faida alisema lengo la harambee hiyo ni kupata fedha kwa ajili ya kujenga msikiti huo.
“Tuna ujenzi wa msikiti, ili ukamilike zinahitajika shilingi milioni sitini na nane laki tisa na arobaini na mbili elfu hivyo tunaomba utuongozee harambee ya kupata fedha hizo,” alisema Imam huyo.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa msikiti mkuu wa eneo hilo Faida, alisema unahahitaji gypsam boards 40 pamoja na uzio wa tofali ili kuweka usalama na utulivu wa ibada na mafunzo ambapo zinahitaji jumla ya shilingi milioni 4,260,000.
Aidha, alisema wanahitaji nyumba mbili za walimu wanaofanya kazi ya kutoa mafunzo na malezi ya kiroho kwa watoto ambapo zinahitajika shilingi milioni 11.6.
“Tunakuomba usimamie zoezi la harambee ili tuanze safari ya kutafuta shilingi milioni 84,802,000 na wafadhili ili waweze kutusaidia juu ya mradi wa shule na kituo cha yatima.” alisema Faida.
Akijibu risala hiyo, Mhandisi Dagaki aliwashukuru waandaaji wa harambee hiyo kwa heshima waliyompa ya kuwa mgeni rasmi kwa kuzingatia kuwa ni kijana wao mzaliwa wa kata hiyo hivyo asingeubeza mualiko huo.
Katika kuchangia ujenzi wa msikiti huo alitoa shilingi milioni 1 na mifuko 20 ya saruji ambapo zaidi ya sh.milioni 2.8 zilipatikana katika harambee hiyo.
Mhandisi Felix Dagaki alitumia nafasi hiyo kuwaoma wanachi wa kata hiyo kujitokeza kuchangia ujenzi wa msikiti huo.