************************************
Na Veronica Mwafisi, MOHA-Dar es Salaam
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya
Huduma kwa Wakimbizi, kesho Desemba 3, mwaka huu,
itafanya uzinduzi wa kuhuisha takwimu za wakimbizi waishio
jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo utafanyika katika Ukumbi wa Polisi Officer’s
Mess, Oysterbay, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Huduma kwa Wakimbizi katika
Wizara hiyo imefafanua kuwa, uhakiki huo utafanywa na idara
hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
“Uhuishaji takwimu utahusisha wakimbizi wote waishio Dar es
Salaam wenye nyaraka, walioruhusiwa kuishi nje ya kambi za
wakimbizi na maeneo mengine kuanzia saa 2 asubuhi,”
ilifafanua taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya uzinduzi uhuishaji
takwimu utafanyika katika Ofisi za Shirika la Relief of
Development Society (REDOSO).
Ofisi hizo zipo Kinondoni, Biafra ambapo wakazi, waombaji
hifadhi wote pamoja na familia zao, wanapaswa kufika ili
kuhuisha takwimu zao bila kukosa.
Mkimbizi yeyote ambaye hatajitokeza wakati wote wa uhuishaji
takwimu taarifa zake hazitahuishwa na usajili wake utasitishwa.
Wakimbizi hao wametakiwa kufika na nyaraka za utambulisho
zikiwemo barua ya uthibitisho wa mkimbizi, usajili, kibali cha
kuishi nje ya kambi, vyeti vya kuzaliwa.
Nyaraka nyingine ni vyeti vya ndoa, hati ya kusafiria,
vitambulisho vya kazi, shule, chuo na nyaraka nyingine yoyote
inayomtambulisha mkimbizi ambayo inatambulika kisheria.
“Shughuli zote zinazohusiana na uhakiki wa taarifa za mkimbizi
na waomba hifadhi zinatolewa bure.
“Uhuishaji huu hautahusisha wakimbizi wa mwaka 1972
wanaotoka makazi ya Ulyankulu, Katumba, Mishano na waishio
vijijini mkoani Kigoma,” ilieleza taarifa hiyo.