Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga akiongea na Wahariri wa vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali ya mfuko huo, Leo 02/12/2019 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) Bw. Christopher Mapunda akiwasilisha mada kwa Wahariri wa vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali ya mfuko na kuanzishwa kwa vifurushi via Bima ya Afya, Leo 02/12/2019 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga Akiwa katika picha ya Pamoja na Wahariri wa vyombo vya habari, Leo 02/12/2019 Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini wakisikiliza uwasilishaji wa mada mbalimbali kuhusu Maendeleo ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na uanzishwaji wa Vifurushi vya Bima ya Afya.
……………….
Na Mwandishi Wetu.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema upo imara na unaweza kujiendesha na kutoa huduma kwa wanachama wake hadi mwaka 2024 bila kupokea michango yoyote kutoka kwa wanachama
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga kwenye mkutano kati ya Mfuko na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari uliofanyika Dar es Salaam leo, kuelezea manufaa ya mpango wa vifurushi vipya
“Naomba niseme wazi kuwa Mfuko haujayumba wala kutetereka kifedha kama inavyodaiwa, tathmini ya Uhai wa Mfuko inaonesha tunao uwezo wa kuwahudumia wanachama wetu kuanzia sasa mpaka mwaka 2024 bila kupokea michango yoyote kutoka kwa wanachama, hivyo madai yanayoenezwa sio ya ukweli,” alisema Bw. Konga.
Alisema kuwa madai ya ucheleweshaji wa kulipa madai kwa baadhi ya watoa huduma hayatokani na kukosa fedha za kulipa bali inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kujiridhisha kwa madai hayo.
“Kuna sababu nyingi za kuchelewesha madai, yapo madai yanakuja na viashiria vya udanganyifu hayo huwezi ukalipa mapema ni lazima uhakikishe umejiridhisha ili ulipe fedha halali na ulinde fedha za wanachama zisitumike isivyo halali,” alisisitiza Bw. Konga.
Akizungumzia uanzishwaji wa vifurushi vipya, alisema kuwa vifurushi hivyo vina lengo la kuwahakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu wananchi wote watakaojiunga na mpango huo.
Alisema kuwa vifurushi hivyo vimebeba huduma zote za matibabu ya msingi ambayo mwananchi aliyejiunga na vifurushi hivyo ana uwezo wa kupata huduma za matibabu katika vituo vyote vilivyosajiliwa na Mfuko Tanzania Bara na Zanzibar.
“Mfuko haujabuni vifurushi hivi kwa lengo la kuongeza mapato ya Mfuko. Vifurushi ni kwa ajili ya kifikia watanzania wengi walio katika sekta binafsi ambao hawana fursa yoyote ya kupata bima binafsi hivyo niwatoe wasi wasi wananchi juu ya mpango huu, ni mpango ambao una manufaa kwa ajili ya afya za wananchi,” alisema Bw. Konga.