Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula akizungumza kwenye siku ya Ukimwi duniani ambapo katika Mkoa wa Manyara, imefanyika Mji mdogo wa Mirerani.
Mkurugenzi wa Tanzanite Founder Foundation, Asha Ngoma (kushoto) akizungumza kabla ya kuanza kwa mbio fupi kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambapo kwenye Mkoa wa Manyara imefanyika Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro wakishindana kuvuta kamba na wanajeshi wa JWTZ kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambapo katika Mkoa wa Manyara, zilifanyika Mji mdogo wa Mirerani.
***************************************
Wakazi 4,076 wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamepima magonjwa mbalimbali katika kuadhimisha siku ya ukimwi duniani yenye kauli mbiu ya jamii ni chachu ya mabadiliko tuungane kupunguza maambukizi mapya ya VVU.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula akizungumza kwenye maadhimisho hayo ambayo kimkoa yamefanyika mji mdogo wa Mirerani jana alisema wananchi hao wamejitokeza kupima magonjwa tofauti.
Chaula alisema waliopima VVU ni 2,739 wakiwemo wanawake 1,168 na wanaume 1,571 na waliogundulika na virusi ni 98 sawa na asilimia 3.6.
Alisema waliofanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu (TB) ni 337 wakiwemo wanaume 139 na wanawake 198 ila bado majibu hayajatoka.
Alisema wanawake 178 walifanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na 68 wakakutwa na dalili za kansa na walipatiwa tiba ya mgandisho papo hapo.
“Watu 78 walipimwa magonjwa ya zinaa na 11 wakakutwa na maambukizi, wanawake 226 walipata huduma ya uzazi wa mpango, watu tisa walichangia damu na watu 507 walipima uzito na urefu,” alisema.
Mkurugenzi wa Tanzanite Founder Foundation, Asha Ngoma, ambaye ni mmoja kati ya waandaaji wa maadhimisho hayo aliwashukuru wote walioshiriki kuyafanikisha ikiwemo serikali.
Ngoma alisema lengo lao ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa watoto wachimbaji wa madini, wamiliki wa migodi na wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayozunguka migodi juu ya suala la afya na usalama maeneo ya kazi.
Alisema wananchi wengi walishiriki maadhimisho hayo ikiwemo maandamano, kuvuta kamba, kukimbia mbio fupi, kusikiliza mashairi, ngojera, nyimbo, hotuba na ujumbe wa kupiga vita maambukizi mapya ya VVU.
Hata hivyo, aliomba radhi endapo kumetokea mapungufu kwenye maadhimisho hayo kwani jambo lolote lililopangwa kwa ajili yao lilikuwa ni geni hivyo watajifunza kwenye wakati mwingine.
Kaimu mratibu wa ukimwi mkoani Manyara, Scola Mwalyanzi alisema lengo la kufikia 90 tatu kwenye mkoa huo litatimia ifikapo mwaka 2020.
Mwalyanzi alisema mkoa wa Manyara unaonyesha kiwango cha maambukizi ya VVU kimeongezeka kutoka asilimia 1.5 mwaka 2011/2012 na kufikia asilimia 2.3 mwaka 2016/2017.