N/Waziri wa Viwanda na Biashara Eng. Stellah Manyanya (wa pili Kushoto) akitoa maelekezo kwa Msajili wa Bodi ya Usajili Wataalamu wa Miapango Miji nchini Hellen Mtutwa (Kulia) wakati alipotembelea mabanda ya maonesho katika Mkutano wa Wataalamu wa Mipango mwishoni mwa wiki.
N/Waziri wa Viwanda na Biashara Eng. Stellah Manyanya (katikati) Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji Profesa Wilbert Kombe (Kushoto) na Msajili wa Bodi ya Wataalamu wa Mipango Miji Hellen Mtutwa ( kulia) wakiwasili katika Mkutano wa Wataalamu wa Mipango Miji Nchini uliofanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.
N/Waziri wa Viwanda na Biashara Eng. Stellah Manyanya (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wataalamu wa Mipango Miji na baadhi ya wajumbe kwenye Mkutano wa Wataalamu wa Mipango Miji Nchini uliofanyika
Mwishoni mwa wiki jijini Dodoma. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
………………..
Na Munir Shemweta, WANMM DODODMA
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stellah Manyanya ametaka kushirikishwa kwa sekta ya ardhi hasa idara ya Mipango Miji katika miradi mbalimbali inayoibuniwa na serikali ili kuondokana na miradi isiyokuwa na tija kwa jamii.
Mhandisi Stellah Manyanya aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano mkuu wa sita wa Mwaka wa Wataalaamu wa Mipangomiji uliofanyika jijini Dodoma.
Alisema, kumekuwepo na miradi mingi nchini inayoanzishwa na Serikali na kutumia gharama kubwa lakini matokeo yake imekuwa haitumiki ipasavyo na wakati mwingine inaingiliana na shughuli nyingine za kijamii hali inayosababisha kuzuka kwa migogoro kwenye jamii.
Alitolea mfano Jengo la Machinga Complex lililopo Ilala Jijini Dar es Salaam, Mhandisi Manyanya alisema, kutokuwepo kwa mipango kina ya muda mrefu na utafiti duni ndio chanzo kikubwa hadi leo jengo hilo limeshindwa kufikia lengo walilojiwekea la kuwasaidia wafanyabiashara wadogowadogo katika shughuli zao.
“ Kuna wale wenzetu waliojenga lile Jengo kubwa kabisa wakalipa jina la heshema Machinga Complex lakini kwa namna walivyopanga na kutumia fedha kwenye kujenga limebaki kuwa jengo la aibu” Alisema Mhandisi Stellah Manyanya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Wilbert Kombe alisema, Miradi Mingi nchini inafanyika bila kushirikisha wataalamu wa Mipangomiji kwani Taasisi nyingi za Serikali zinapopanga mipango yake ya kiuchumi na miundombinu hazizingatii na kuonesha mipango ya ardhi hali inayosababisha muingiliano wa shughuli za kiuchumi.
Aliongeza kwa kusema kuwa, Taasisi zote nchini zinategemea uwepo wa ardhi, hivyo hazina budi kushirikiana na Sekta zote zinazohusu ardhi kabla ya kupanga mipango yao ya kiuchumi ili kuepusha muingiliano na kupangwa vibaya kwa miji.
‘’Ukitazama eneo la Maegesho ya magari ya Mwendokasi eneo la Jangwani Jijini Dar es Salaam , hayo ni matokeo ya kutoshirikishana katika mipango miji kwani lilile eneo linahitaji mambo mawili ama lihamishwe au iinuliwe barabara kuanzia Magomeni “ Alisema Profesa Kombe.
Naye Msajili wa Bodi ya Wataalamu wa Mipango Miji Hellen Mtutwa alisema, taasisi zote za Serikali ni lazima ziwe na ushirikiano wa karibu wakati wa kuandaa mipango na kuitekeleza siyo sekta za ardhi tu bali Tanesco ,Tanroad Maji na taasisi nyingine ili kuepusha hasara kwa Serikali .
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa City Plan Consultants (T) Limited Dkt Juma Mohamed alisema, maendeleo yote yapo kwenye sekta ya ardhi hivyo Serikali inatakiwa iipe kipaumbele sekta hiyo kwani hasara ya kutokufanya mipango ni kubwa kuliko kuitekeleza.