Tanki la Maji lililopo Kongwa mjini
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa (katikati mwenye miwani ) akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua mradi wa maji kijiji cha Vihingo wilayani Kongwa Mkoani Dodoma
Mkuu wa wilaya ya Kongwa Deogratius Ndejembi,akisisitiza jambo kwa wananchi akiwa na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa (katikati mwenye miwani ) mara baada ya kukagua mradi wa maji kijiji cha Vihingo .
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa (katikati mwenye miwani ) akiwa na Mkuu wa wilaya ya Kongwa Deogratius Ndejembi,wakimsikiliza Meneja wa RUWASA wilaya ya Kongwa Mhandisi Kaitaba Lugakingira (kushoto) wakati wa ziara ya waziri kukagua miradi ya Maji kijiji cha Vihingo.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa Tanki la Maji lililopo katika kijiji cha Vihingo wilayani Kongwa Mkoani Dodoma.
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa (katikati mwenye miwani ) akifafanua jambo kwa wananchi mara baada ya kukagua mradi wa maji kijiji cha Vihingo wilayani Kongwa Mkoani Dodoma.
Sehemu ya watendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibaigwa wakifatilia hotuba ya Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa ambaye alifanya ziara ya kukagua miradi ya maji katika wilayani ya Kongwa jijini Dodoma.
Waziri wa Maji Mhe.Profesa Makame Mbarawa ,akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibaigwa mara baada ya kukagua miradi ya Maji iliyopo wilayani Kongwa Mkoani Dodoma.
……………..
Na.Alex Sonna,Kongwa
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa amewataka Mameneja wa Mamlaka za Maji kuhakikisha wanaongeza mitandao ya maji kwa wananchi sambamba na kuimarisha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na matumizi ya maji kwa wananchi na taasisi mbalimbali.
Pia amesema serikali imejipanga kuhakikisha wanatatua changamoto za maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini, huku akiwataka wataalamu wa kusoma mita kufanya kazi kwa weredi kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuepuka kuhujumu mapato.
Waziri Profesa Mbarawa ameyasema hayo akiwa katika Mji mdogo wa Kibaigwa Wilayani Kongwa, Mkoani Dodoma, wakati akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Maji ya mji mdogo wa kibaigwa, katika ziara ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa katika Wilaya ya Kongwa.
Amesema serikali imejipanga kuhakikisha wanamaliza tatizo la maji na ni lazima Mamlaka zihakikishe zinaongeza mitandao ya maji kwa wananchi na kusimamia ukusanyaji wa mapato na hata sita kuwaondoa wale wanaozembea katika kusimamia miradi ya maji na kuhujumu mapato ya maji na kashaanza kuwaondoa na ataendelea kuwaondoa.
“Tatizo la Mameneja wengi wanakuwa na mitandao midogo ya usambazaji wa Maji kwa wananchi, Serikali tumejipanga hakikisheni mnaongeza mitandao ya maji kwa wananchi mapato yaweze kupatikana Mimi ninachoangalia ni ukusanyaji wa mapato Sina ndugu ninachotaka mapato yakusanywe”
“Na ninyi watumishi mnapoenda kusoma mita msidanganye na tabia ya kuwaunganisha wateja maji kinyemela msifikili naweza kuwa toa hao tu hata ninyi nitawatoa kwenye nafasi zenu, nimeshabadilisha uongozi katika maeneo Kama Moshi, Mbeya na Arusha na nitaendelea mpaka nione Mamlaka hizi zinajitegemea” amesema Waziri Mbarawa.
Waziri Mbarawa akiwa katika mradi wa Maji wa Mtanana B, mradi ambao umekamilika na vituo 11 Kati ya 14 vimekamilika na wananchi tayari kuanza kupata huduma za maji, amemtaka Mhandisi wa Maji kuhakikisha anasimamia Jumuiya ya maji nakuwafahamisha majukumu yao katika kusimamia Jumuiya za maji ili ziweze kuleta tija kwa wananchi.
“Miradi Kama hii iliyokamilika nataka Wahandisi mhakikishe mnaweka usimamizi madhubuti na muweke Jumuiya za maji zilizoimara na kuwafahamisha majukumu yao na sio kila fedha inayopatikana kwenye miradi hii zinatumika ovyo”
Aidha akiwa katika Mradi wa Maji wa Vihingo, ambao ulitakiwa kuwa umekamilika lakini bado haujakamilika amempongeza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kongwa Mhandisi Kaitaba Lugakingira, kwa kuendelea kumbana mkandarasi huyo wa mradi wa kampuni ya MSHAMINDI kuhakikisha anamaliza mradi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Deogratus Ndejembi, mbali na kumshukuru Waziri kwa kuendelea kuimarisha huduma za maji, amemuomba kumuongezea bajeti Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kongwa, ili mradi wa Maji wa Vihingo usambae mpaka Kijiji Cha Lengaji, ambacho kipo karibu na mradi ulipo nao waweze kupata huduma za maji.
Katika ziara hiyo Waziri Prof. Mbarawa ametembelea katika miradi ya maji ya Kongwa Mjini, Vihingo na Mtanana B, pamoja na kuzungumza na watumishi wa Mamlaka ya Maji ya Mji Mdogo wa Kibaigwa.