*************************************
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ni moja ya washiriki kwenye mashindano ya SHIMMUTA yanaoendelea Mkoani Mwanza. Mashindano hayo yamefunguliwa rasmi leo tarehe 30.11.2019 katika viwanja vya Nyamagana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Philis Nyimbi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Waziri alihamasisha na kusisitiza taasisi za umma na makampuni binafsi kushiriki kwa wingi katika mashindano hayo kwani afya ni mtaji mkubwa sana kwa wafanyakazi.
TBS mpaka sasa inaendelea kufanya vizuri kwenye mashindano hayo haswa katika michezo ya mpira wa miguu, mpira wa wavu na kuvuta kamba. Vile vile TBS imechukua fursa ya kushiriki mashindano haya kwa kwenda sambamba na kutoa elimu ya masuala ya viwango kupitia vyombo mbalimbali vya kijamii katika kanda ya ziwa hususani mwanza ili kuhakikisha soko la Tanzania linakuwa na bidhaa bora na salama.
Jumla ya Taasisi/ Mashirika na Kampuni 46 zimeweza kushiriki SHIMMUTA 2019 na Kauli mbiu ya mashindano mwaka huu ni ” Wafanyakazi wenye Afya ni Chachu ya Maendeleo ya Viwanda. Tushiriki Michezo kwa Ustawi wa Afya za Wafanyakazi na Maendeleo ya Taifa”.