Home Mchanganyiko TARURA watakiwa kushughulikia maeneo korofi msimu wa mvua

TARURA watakiwa kushughulikia maeneo korofi msimu wa mvua

0

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele) akitoka kuangalia daraja la mto Kanteza linalowaunganisha wananchi na kituo cha afya cha Laela, Wilayani Sumbawanga, daraja ambalo limetengewa shilingi milioni 163.2 katika mwaka wa fedha 2019/2020 huku kazi zikiwa zinaendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele) akitoka kuangalia daraja la mto Kanteza linalowaunganisha wananchi na kituo cha afya cha Laela, Wilayani Sumbawanga, daraja ambalo limetengewa shilingi milioni 163.2 katika mwaka wa fedha 2019/2020 huku kazi zikiwa zinaendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akizungumza na baadhi ya wananchi wa mji mdogo wa Laela juu ya adha wanayoipata kabla ya dalaja la mto Kanteza kuanza kutengenezwa na kutaka kujua maoni yao juu ya ujenzi huo muda mfupi baada ya kukagua daraja hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimkabidhi zawadi ya pesa mmoja wa mtoto wa wananchi aliokuwa akizungumza nao kupata maoni juu ya ujenzi wa daraja la mto Kanteza katika mji mdogo wa Laela.

********************************

Wakala wa Barabara za mijini na Vijijini (TARURA) wametakiwa kuhakikisha Barabara zote za Vijijini zinapitika mwaka Mzima kwa kufanyiwa matengenezo na endapo itashindikana basi ni muhimu kuyapa kipaumbelea maeneo korofi, hasa katika kipindi hiki cha Mvua jambo ambalo litawasaidia wananchi kuendelea na shughuli zao za Kiuchumi bila vikwazo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo katika kikao cha Bodi ya barabara baada ya wabunge wa mkoa huo pamoja na wenyeviti wa halmashauri kuilalamikia TARURA juu ya utendaji wake wa kazi pamoja na mipangilio yao ya bajeti katika kutekeleza majukumu yao.

“Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA) kuhakiki Barabara zote za vijijini katika Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa ili kwanza wawe na orodha kamili ya Barabara za Vijijini na  zipo kwenye hali gani,Baada ya kuhakiki wawe na orodha ya Barabara zilizoingizwa kwenye Mtandao wa  Barabara za TARURA na Barabara zipi hazipo kwenye mtandao wa Barabara za TARURA na kwanini?,” Alihoji

Aidha alisema kuwa kwa kufanya hivyo itawasaidia TARURA kuwa na picha ya Barabara zote za Mkoa wakati wa upangaji wa Bajeti ya mwaka 2020/2021 ili waweze  kuziweka kwenye Bajeti Barabara ambazo zinahitaji Matengenezo.

Wakati wakiwasilisha malalamiko hayo miongoni mwa wabunge hao walisema kuwa hawaridhishwi na bajeti inayotengwa na TARURA na hata hiyo inayotengwa haifikishwi kwa wakati hali ambayo inasababisha hata hicho kidogo kilichotengwa kushindwa kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mh. Ali Kessy alisema, “Tumepanga bajeti milioni 400 wazilete zote milioni 400, hauwezi kupanga bajeti milioni 400 unaleta milioni 20, nimemuuliza mratibu wa (TARURA) Mkoa, mmeleta shilingi ngapi anasema tumeleta milioni 20 kwenye bajeti ya serikali ya milioni 400, walitenga kabia daraja la Kavunje, wakadarasai wamekwama daraja haliendelei na mvua ndio hiyo kama unavyoona.”

Naye Mbunge wa Nkasi Kusini Mh. Desderius Mipata alisema kuwa wananchi wa kata ya Ninde watatengwa kutokana na TARURA kushindwa kutenga bajeti kwaajili ya ukarabati wa barabara inayowaunganisha wananchi wa kata hiyo na kata za jirani.

“Kwahiyo naomba mtafute njia yoyote ya dharura ya kuwezesha eneo hilo lipitike hakuna namna nyingine ya kufanya, nikiwa bungeni daraja la kwenda ninde lilikuwa limevunjika, nikapiga kelele bahati nzuri walikuja wakatengeneza kwa pesa kidogo lakini barabara yake haipitiki,” Alimalizia.

Wakati akitoa malalamiko yake kwa niaba ya wakandarasi wenzie Bwana Anyosisye Kiluswa amesema kuwa wakandarasi bado wanazidai halmashauri fedha za matengenezo ya barabara kadhaa kabla ya barabara hizo hazijahamishiwa kwa TARURA na kuongeza kuwa halmashauri hizo zilishapewa fedha na serikali lakini matokeo yake wametumia kwa matumizi mengine.

“Sasa kwa sasa hivi wakandarasi tunashindwa kutekeleza wajibu wa kufanya kazi kwasababu pesa zetu wenyewe ni za kuunga unga, ukifanya kazi umelipwa halafu pesa hiyo hiyo unaichukua unakwenda kufanya kazi sehemu nyingine, sasa unapokuwa unafanya kazi bila ya kulipwa na nyingine ambazo zipo wanazitumia kwenye maeneo mengine matokeo yake wakandarasi wa mkoa wa Rukwa tunaonekana hatufanyi kazi vizuri,” Alisisitiza.

Kwa upande wake Kaimu mratibu wa TARURA Mkoa wa Rukwa alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya fedha shilingi bilioni 4.133 kwaajili ya matengenezo ya barabara km 346.63 na vivuko 48 huku kutoka mfuko wa barabara zikitengwa shilingi bilioni 1.763 kwaajili ya miradi ya maendeleo ambapo daraja la mto Kavunja likitengewa shilingi milioni 400 na daraja la mto Kanteza lilopo Laela likitengewa shilingi milioni 163.2.