Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akitembelea jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya leo. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe.Dkt. John Utamwa
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe.Dkt. John Utamwa. |
1(Na. Rajabu Singana, Mahakama Kuu Mbeya)
……………
Na. Rajabu Singana, Mahakama Kuu Mbeya
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema kwamba Tanzania ina mgawanyo wa madaraka na unaofuatwa vizuri tofauti na nchi nyingine.
Akizungumza leo Novemba 28,mwaka huu wakati alipotembelea Ofisi za Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Waziri Mahiga alisema ametembea nchi mbalimbali na kujifunza kwamba katika nchi yetu mgawanyo wa madaraka (separation of power) unafuatwa.
‘Mgawanyo wa madaraka kwa mihimili ya dola, ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama upo na unafuatwa vizuri kulinganisha na nchi nyingine ambapo hata kuonekana haionekani kabisa na kama ilikuwepo basi ilikufa, alisema Waziri Mahiga.
Akizungumzia kuhusu kazi kubwa inayofanywa na Wahe. Majaji ya kusikiliza mashauri ambapo kuna wakati wanalazimika kufanya kazi hadi kwa zaidi ya saa 18 kwa siku ili kuweza kuwahudumia wananchi na kufikia malengo ya kitaasisi, alisema anatambua mchango huo na kuwapongeza.
Pamoja na pongezi hizo, amewataka majaji hao, kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na utendaji uliotukua kiasi kwamba ikitokea mtu ameulizwa haki ni nini? katika kutoa majibu amchukue Jaji na kusema hii ndio maana ya haki.
Hivyo katika hilo amewashauri Wahe. Majaji kuwa na maadili ya ziada na kuufanya Mhimili wa Mahakama kutekeleza majukumu kwa viwango vya juu.
Vile vile Waziri Mahiga amesema kupitia kuongezeka kwa watu na kukua kwa Sayansi na Teknolojia, nchi yetu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha watu kubuni njia nyingi za uhalifu.
Alisema changamoto hizo zinasababisha kuwa na uhaba wa majaji kitendo kinachowalazimu kuwa na makadirio ya kusikiliza mashauri mengi zaidi tofauti na mipango ya kitaasisi, na kila mmoja kulazimika kufanya kazi kwa muda mrefu.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Dkt. John Utamwa, alisema mikakati ambayo imekuwa ikitumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya katika kuhakikisha mashauri yanaamuliwa kwa wakati na ubora unaotakiwa ni uwepo wa miongozo mbalimbali juu ya utoaji huduma kwa mfano kabla ya kufika siku 21 nakala za hukumu zinatakiwa kuwa tayari lakini Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Nakala za Hukumu hutolewa ndani ya siku ambayo hukumu hutolewa.
Waziri wa Sheria na Katiba yupo katika ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, ameambatana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Mhe. Biswalo Mganga ambapo wakikagua Magereza na kutambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafungwa na Mahabusu.
Katika ziara hiyo, Mhe. Biswalo Mganga amewafutia mashtaka jumla ya watuhumiwa 47.