Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongea na viongozi wapya wa vijiji na vitongoji muda mfupi baada ya viongozi hao kula kiapo.
Baadhi ya Wenyeviji wa vijiji, vitongoji, viti maalu na wajumbe mchanganyiko wakila kiapo wakati wa hafla fupi ya uapisho wa viongozi hao iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (hayupo Pichani) tarehe 29.11.2019.
Baadhi ya Wenyeviji wa vijiji, vitongoji, viti maalu na wajumbe mchanganyiko wakila kiapo wakati wa hafla fupi ya uapisho wa viongozi hao iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (hayupo Pichani) tarehe 29.11.2019.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimsalimia baadhi ya wenyeviti wa kijiji muda mfupi kabla ya kuondoka eneo hilo baada ya viongozi hao kula kiapo tayari kwa kuwatumikia wananchi katika maeneo yao.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimkabidhi zawadi motto wa mmoja wa wenyeviti wa vitongoji muda mfupi kabla ya kuondoka eneo hilo baada ya viongozi hao kula kiapo tayari kwa kuwatumikia wananchi katika maeneo yao.
……………….
Viongozi wapya 2,766 wa vijiji na vitongoji walioshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika tarehe 24.11.2019 katika wilaya ya Kalambo wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanatatua kero na malalamiko ya wananchi wanaowahudumia katika vijiji na vitongoji ili kupunguza msongamano wa wananchi wanaohitaji kutatuliwa kero zao katika ngazi ya wilaya na mkoa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo muda mfupi baada ya viongozi hao kula kiapo mbele yake na mbele hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Kalambo ambapo wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutoka katika kata 10 za tarafa ya Matai wilayani humo walishiriki katika kiapo hicho.
“Katika ngazi hiyo ya vijiji, vitongoji na mitaa, wenyeviti wa maeneo hayo mimi nikipata mtu anatoka kwenye vijiji vyenu analalamika kwa jambo ambalo ni dogo sana, nitakuita. Utapata usumbufu wa kuja Sumbawanga, uhisabu kuwa utatumia gharama zako kuja na kurudi kutoka kule kweny kijiji chako. Nitakusumbua kwasababu wewe hutaki kusumbuka nikilipata tu nitakusumbua, kwahiyo nendeni mkatatue kero za wananchi katika ngazi zenu, yako mambo mengi mtusaidie sio kila kitu mkuu wa mkoa, kila kitu mkuu wa Wilaya na wengine wanakwenda wanaandika mpaka kwa Rais,”Alisisitiza.
Aidha amewataka viongozi hao kuwaumikia wananchi wote bila ya kujali vyama vyao vya kisiasa, dini wala kabila na kuwataka katika utekelezaji huo kuwa shirikishi kwani wasipofanya hivyo wananchi watashindwa kushiriki katika shughuli za kimaendeleo jambo litakalorudisha nyuma juhudi za mkoa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma stahiki na kwa wakati.
“Mambo ambayo mnapaswa kwenda kuyasimamia katika maeneo yenu kuwashirikisha wananchi katika kupanga maendeleo, sio unakurupuka tu unasema mimi nataka hiki kifanyike bila ya kuwashirikisha wananchi , lazima wapange waamue wao wenyewe na wakishaamua wao wenyewe watashiriki katika kutekeleza lakini pia watasimamia kulinda yale maamuzi yao na hiyo ndio demokrasia na hili ndilo mkalifanye kule, viongozi wengine wakishachaguliwa kama hivi wanakuwa miungu watu, hatupendi kuona miungu watu kwenye vijiji vitongoji na mitaa,” Alisema.
Na katika kuhakikisha viongozi hao wanatekeleza majukumu yao bila ya visingizio amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri nne za mkoa huo kuwapatia mafunzo viongozi hao wapya pamoja na wale ambao ni muhula wao wa pili au zaidi jambao litakalotawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa Mujibu wa Sera za Kisekta, Mikakati ya Kisekta, Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu zinazosimamia Sekta husika.
Wakati akitoa muhtasari wa taarifa ya uchaguzi wa serikali za mitaa mratibu wa uchaguzi mkoa Albinus Mgonya alisema kuwa mitaa 165 iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga imechukuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo ni sawa na asilimia 100 wakati katika ngazi ya vijiji CCM imechukua vijiji 336 huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikichukua vijiji 2 kati ya vijiji 339 vya mkoa wa Rukwa.
“Vitongoji vilivyoshiriki katika uchaguzi ni 1,816 na kwa nafasi ya vitongoji Chama cha Mapinduzi kimepata nafasi 1,807 sawa na asilimia 99.4 Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimepata nafasi za wenyeviti wa vitongoji 8 sawa na asilimia 0.6. kwa faida ya wadau waliopo hapa nafasi hizi 8 mgawanyo wake ni kama ifuatavyo, Sumbawanga Manispaa nafasi 1, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga nafasi 1 na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi nafasi 6,” Alimalizia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mh. Daudi Sichone wakati akitoa neon la shukurani aliwataka viongozi hao wapya kuhakikisha wanawapatia elimu ya kutosha wananchi wanaowaongoza juu ya kutatua kero na malalamiko katika ngazi hizo zao na sio kumshawishi mwananchi afike ngazi mkoa.
“Hawa viongozi wetu wanantumia mkoa na taifa, hebu ifike mahali tutoe elimu kwa wananchi wetu, kabla hajafika huko angalau akifika kule ionekane sisi sote tunasapoti kwamba kwa tatizo lako hili ni vyema ukafika kwa mkuu wa mkoa lakini sio tu unaamka tu na masimu yako unamyuhangaisha mzee wa watu anashindwa kufanya kazi za watu,”Alisema.
Maeneo yaliyofanya uchaguzi katika mkoa wa Rukwa ni vijiji 67, vitongoji 348, mitaa 9 na wananchi walioshiriki kupiga kura ni 118,887 huku zoezi hilo la uchaguzi likiwa limefanyika katika hali ya amani na utulivu.