Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati aliwasili kwenye kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Novemba 29, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha IFM, Dkt. Benson Bana, wakati aliwasili kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Novemba 29, 2019. Katikati ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa anaingia kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha, yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. ,Novemba 29, 2019.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, akizungumza na Wahitimu wa Chuo cha IFM, kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. ,Novemba 29, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia Wahitimu wa Chuo cha IFM, kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. ,Novemba 29, 2019.
Wahitimu wa Chuo cha IFM, wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati akiwahutubia kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. ,Novemba 29, 2019
……………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kukusanya mikopo iliyoiva yenye thamani ya shilingi bilioni 183.3 sawa na asilimia 116.2 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 157.7.
“Natambua kwamba baadhi ya wahitimu wamepata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, hivyo natumia fursa hii kuwakumbusha wale wote mlionufaika na mkopo wa Serikali katika kutimiza ndoto zenu za kupata elimu ya juu, mkumbuke kurejesha mikopo,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Novemba 29, 2019) wakati akizungumza kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila anayenufaika na mkopo asaidie wengine walio nyuma yake ili nao waweze kufaidika na utaratibu huo wa kukopa na kulipa. Alisisitiza kwamba bila kufanya hivyo, ni ukweli usiopingika kuwa Serikali itashindwa kuwajengea uwezo wananchi wake wa kupata fursa zinazojitokeza za elimu katika ngazi mbalimbali.
“Ikumbukwe kuwa, maendeleo ya Taifa lolote yanategemea uwekezaji katika rasilimali watu. Hivyo nitoe rai kuwa wote mliokopeshwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu mfanye hima kulipa,” alisema Majaliwa
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wahadhiri na wanachuo wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu vilivyopo Dar es Salaam wachangamkie fursa ya kupata nyumba na vyumba vya kupangisha katika miradi ya ujenzi wa nyumba ya NSSF, NHC na Watumishi Housing zilizopo Kigamboni.
Amesema amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF atenge maghorofa ambayo yatakaliwa na wahadhiri na wanafuzi wa vyuo vya elimu ya juu na vyuo vikuu tena waache kuwatoza bei kubwa na badala yake wapange bei mpya za kupangisha ambazo wanachuo watazimudu.
Ili kufanikisha utekelezaji wa jambo hilo, Waziri Mkuu amesema amewashauri viongozi wa taasisi za elimu ya juu za mkoa wa Dar es Salaam wafanye mawasiliano na Watendaji Wakuu wa NSSF, NHC na Watumishi Housing ili wafikie makubaliano ya namna ya kupangisha au kununua nyumba hizo.
Akizungumzia suala la kuboresha usafiri kwa wanafunzi na watu wakaoishi kwenye nyumba hizo, Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari amekwishatoa maelekezo kwa viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam wakiwemo Wakuu wa Wilaya za Kigamboni na Temeke wakutane na uongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) ili wapange safari za mabasi ya abiria kutoka Tuangoma, Mtoni Kijichi hadi eneo la Ferry Kigamboni.
Mheshimiwa Majaliwa amewasihi wahadhiri na wanachuo wachangamkie fursa hiyo ili waweze kupata nyumba bora za kupanga au kununua ili kuepuka adha ambayo imewakabili kwa muda mrefu ya kupanga au kuishi katika nyumba duni.
Akiwaasa wahitimu wa Mahafali hayo, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Mnao wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa mnatumia vizuri elimu mliyoipata chuoni ili kuchochea maendeleo ya kweli ya nchi yetu. Hivyo basi, huko mnakoenda iwe ni kwenye Halmashauri, Mikoa, Wizara, taasisi za umma na hata sekta binafsi, mkawe chachu ya mafanikio.”
“Aidha, mtakapokuwa huko kwenye maeneo mbalimbali ya kazi, hakikisheni mnajitanabaisha kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu. Tunawatarajia muwe mfano kwa kuwa waadilifu, waaminifu na wachapa kazi,” alisema Mheshimiwa Majaliwa.
Aliwasihi wahitimu hao kuwa watakapoingia kwenye utumishi wa umma au kwingineko wakazingatie maadili na kujiepusha na tabia ya kujitafutia utajiri wa harakaharaka. “Kafanyeni Kazi kwa uzalendo wa hali ya juu,” aliongeza Mheshimiwa Majaliwa.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza katika mahafali hayo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango alisema ili Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kiweze kuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, ni lazima uongozi wa chuo hicho utekeleze sera ya elimu kwa vitendo na kuwa wabunifu katika kupitia upya mitaala, ufundishaji na kufanya tafiti.
Waziri Mpango amelitaka Baraza la Uongozi wa Chuo cha IFM na wanataaluma waendelee kuwa wabunifu zaidi ili kuhakikisha kwamba fani zinazofundishwa Chuoni hapo zinaendana na wakati huku wakizingatia mahitaji ya nchi na wananchi wake pamoja na mabadiliko ya haraka ya kitekinolojia yanayoendelea ulimwenguni.
Jumla ya wahitimu 2,775 wametunukiwa tuzo mbalimbali na wanafunzi 20 wa Shahada ya Usimamizi wa Fedha wamepongezwa.