***********************************
Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) wa mkoa wa Kagera, Mh. Oliver Semuguruka,
amewashauri viongozi mbali mbali wa serikali kushirikiana na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika kuboresha mazingira ya kazi hapa nchini.
Ametoa ushauri huo jana alipotembelea ofisi za OSHA zilizopo kinondoni jijini Dar es Salaam ambako alikwenda kufanya mazungumzo na uongozi kwa ajili ya kuweka mikakati ya pamoja ya kuhamasisha uzingatiaji wa viwango vya Usalama na Afya mahali pa kazi kwa watu wenye ulemavu.
“Baada ya OSHA kuniteua kuwa balozi wa watu wenye ulemavu katika masuala
yanayohusu afya na usalama wao, niliona kuna haja ya kuonana na uongozi ili
niweza kufahamu zaidi changamoto za kiusalama na afya zinazowagusa watu
wenye ulemavu na hivyo kuweka mikakati madhubuti ya kuzitatua kwa kushirikiana na OSHA,” alisema Semuguruka.
Aliongeza: “Katika mazungumzo yangu leo na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, nimebaini kwamba OSHA wanafanya kazi kubwa na yenye
changamoto nyingi. Kama kiongozi nimeguswa sana na kazi yao na ningependa
kutumia fursa hii kuwashauri viongozi wenzangu katika maeneo mbali mbali ya nchi waunge mkono juhudi hizi za OSHA katika kuwalinda wafanyakazi dhidi ya
vihatarishi vya kiusalama na afya ambavyo husababisha ajali na magonjwa katika sehemu nyingi za kazi.”
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, alimshukuru Mbunge huyo
kwa kukubali jukumu hilo zito alilopewa pamoja na jitahada ambazo ameanza
kuzifanya ikiwemo kutembelea ofisi za OSHA kwaajili ya kuweka mikakati ya
kutekeleza wajibu huo aliopewa.
Mwishoni mwa juma lililopita OSHA waliandaa na kutoa mafunzo ya Usalama na
Afya mahali pa kazi kwa wanachama wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMVITA) wa mkoa wa Kageara ambapo katika semina hiyo, Mh. Semuguruka aliteuliwa kuwa balozi wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi kwa upande wa watu wenye ulemavu.