Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji Hellen Mtutwa (Kushoto), Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Imaculata Senje na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara Hamdoun Masoor wakiwa katika Mkutano wa Wataalamu wa Mipango Miji Nchini unaoendeleo jijini Dodoma leo tarehe 27 Novemba 2019.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji Profesa Wilbert Kombe (Kushoto), Mkurugenzi wa Kampuni ya City Plan Vicent Shaidi na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam Dkt Dawah Magembe wakiwa katika Mkutano wa Siku tatu wa Wataalamu wa Mipango Miji unaofanyia jijini Dodoma leo 27 Novemba 2019.
Baadhi ya wajumbe wakiwa katika mkutano wa Wataalamu wa Mipango Miji unaoendelea jijini Dodoma leo 27 Novemba 2019.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdoun Mansoor akiwasilisha mada katika mkutano wa Wataalamu wa Mipango miji unaoendelea jijini Dodoma leo tarehe 27 Novemba 2019.
………………
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji Profesa Wilbert Kombe amesema tofauti kubwa kati ya mipango ya kiuchumi na ile ya maendeleo ya ardhi ndiyo chanzo kikubwa cha kutokuwepo miji iliyopangika na kutaka kuwepo ushirikishwaji ili kuwa na miji iliyopangika.
Profesa Kombe alisema hayo leo tarehe 27 Novemba 2019 katika mahojiano maalum wakati wa kikao cha siku tatu cha Wataalamu wa Mipango kinachoendelea jijini Dodoma.
Alisema, kwa sasa mipango, sera na utekelezaji kuhusiana na masuala ya mipango miji vipo lakini tatizo kubwa ni tofauti katika mipango ya kiuchumi na maendeleo kwenye sekta ya ardhi kwa ujumla.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji ambayo iko chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa, tatizo lingine linalochangia suala hilo ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusiana na manufaa wanayoweza kuyapata katika ardhi iliyopangwa
‘’Mtu ukipanga ardhi yako unaongeza thamani hata kabla haijaongezewa huduma nyingine kama vile maji na umeme ndyo maana kuna tofauti kubwa kati ya anayeuza ardhi iliyopangwa na yule ambaye haijapangwa’’ alisema Profesa Kombe.
Alihimiza uwepo wa ushirikiano baina ya Serikali na sekta nyingine katika masuala mbalimbali yanayohusu upangaji miji ili kuepuka kuwa na maeneo yasiyopangwa ambayo mwisho wa siku ni kuwa na makazi holela.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Wataalamu wa Mipango Miji Hellen Mtutwa alisema, Mkutano wa wataalamu wa mipango miji unaoendelea unawakutanisha wataalaumu wote wa mipango miji kutoka serikalini na sekta binafsi ukiwa na lengo la kuboresha mipango miji nchini na kubainisha kuwa msisitizo mkubwa ni ushirikishwaji kwenye mipango ya matumizi ya ardhi.
Kwa mujibu wa Mtutwa, Ushirikishwaji wa sekta mbalimbali katika mipango miji ya maeneo mbalimbali nchini siyo tu utarahisisha masuala ya upangaji miji bali utaepusha hasara kwa wananchi na serikali kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa City Plan Consultants (T) Limited Dkt Juma Mohamed aliiomba serikali kuipa kipaumbele mipango ya maendeleo ya ardhi kwa kuwa ardhi ndiyo kila kitu hususan katika masuala yanayohusu shughuli za binadamu.
Dkt Mohameda alisema, tatizo kubwa kwa wananchi wengi ni kutegemea matokeo ya haraka kwenye sekta hiyo wakati suala hilo linaweza kuhitaji mipango ya muda mrefu hasa katika masuala ya Mipango Kabambe.