*************************************
Na Ahmed Mahmoud Arusha
MBUNGE viti maalum mkoa wa Arusha, Amina Mollel, ameiomba serikali kuboresha miundo mbinu kwenye shule za msingi na sekondari ili kuwajengea mazingira rafiki wanafunzi wenye ulemavu wa viungo waweze kupata maeneo salama ya kujisaidia kuliko hali ilivyo sasa.
Mbunge huyo ametoa kilio hicho Novemba 27 kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa,RCC, alipokuwa akichangia hoja ya Idara ya afya iliyowasilishwa na mganga mkuu wa mkoa, Dakta Wedson Sichelwe, iliyokuwa ikielezea hali ya patikanaji wa dawa mkoani humo.
Mbunge, huyo alisema miundo mbinu iliyopo kwenye shule hizo sio rafiki kwa wenye ulemavu ,ambapo kwenye ziara yake aliyoifanya shule mbalimbali mkoani humo ameshuhudia walemavu wakitaabika kwenda kwenye vyoo .
Alisema hali hiyo inauma kwa kuwa walemavu wanataabika hivyo kutokana na serikali kutekeleza mpango wa chakula bure unatakiwa uende sambamba na uboreshaji wa miundo mbinu rafiki kwa walemavu .
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga, ameiomba serikali kuhakikisha dawa zinawafikia wananchi na kuwaondolea usumbufu wa kupata dawa mara baada vipimo vya magonjwa.
Alisema taarifa ya upatikanaji iliyotolewa na mganga mkuu hailingani na hali halisi ilivyo vijijini ingawa serikali inatoa fedha za dawa na halmashauri zinalipa wazabuni.ambao wamekuwa hawafikishi huduma hizo kwa wananchhi.
Alisema kuna baadhi ya wazabuni hawana uwezo hivyo waangaliwe upya utendaji wao kwa kuwa wanasababisha usumbufu kwa wananchi kwa sababu hawana uwezo na kusababisha mlundikano wa wananchi kusafiri umbali mrefu kusaka dawa.
Kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya ya Longido, Toba Nguvilo, alisema katika kata za Kitumbeine na Girarungwe, wilayani Longido, Zahanati na vituo vya afya vinavyomilikiwa na Kanisa la KKKT kadi za bima ya afya iliyoboreshwa hazipokelewi.
Alisema wananchi wenye kadi za bima iliyoboreshwa wamekuwa wakishindwa kupata huduma ya tiba kutokana na kadi hizo kutokupokelewa wala kukubalika na hivyo kujikuta wakikosa huduma za matibabu.
Kwa upande wake mchungaji Simon Dereva wa KKKT kwa niaba ya askofu Simoni Masangwa, alisema watalishughulikia tatizo ili kadi hizo ziweze kupokelewa na wananchi wapate huduma huduma za matibabu kwa kuwa serikali imeonyesha ushirikiano wa hali ya juu.
Awali akiwakilisha taarifa yake mganga mkuu wa mkoa,Dakta Wedson Sichelwe, alisema kiwango cha upatikanaji wa dawa katika mkoa huo ni asilimia 99% na kuwaondoa hofu wajumbe na wananchi kuwa suala la dawa katika mkoa sio changamoto kama ilivyokuwa siku za nyuma
Wakati huo huo imeelezwa kuwa mkoa wa Arusha una upungufu wa vyumba vya madarasa ya shule za sekondari 262 ,ambapo wilaya ya Meru inaongoza kwa kuwa na upungufu wa vyumba 66 huku wilayua ya Longido ikiwa na upungufu wa vyumba vine tu.
Katibu tawala mkoa wa Arusha, Richard Kwitega, ameyasema hayo alipokuwa akiwakilisha taarifa ya utekelezaji war obo ya pili ya mwaka ya kamati ya ushauri mkoa ya mwaka 2018/19.
Alisema mkoa katika kutekeleza maazimio ya kikao kilichopita cha mwezi Marchi mwaka huu mkoa unaanza mkakati wa kujenga vyumba hivyo vya madarasa kwa shule za sekondari ili kuondoa usumbufu kwa wanafunzi watakaojiunga na kidatoo cha kwanza mwakani.
Kuhusu afya ,alisema Kwitega,amesema kuwa mkoa unaendelea na ujenzi wa hospital za wilaya za Longido, Karatu Ngorongoro na halmashauri ya Jiji la Arusha ,ambapo ujenzi wake upo kwenye kiwango kizuri.
Alisema kikao kilichopita msisitizo ulikuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo Sekretari ya mkoa na mamlaka za serikali za mitaa mwaka 2018/19 mkoa uliidhinishiwa shilingi ,67,570,830,394.10 kwa ajili ya miradi.