KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru Ally, akisindikizwa na wenyeji wake wakiongozwa na Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu Mhe.Haji Omar Kheri baada ya ufunguzi wa Maulid ya kuadhimisha Sherehe ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) Kisiwani Tumbatu.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru Ally,akiwa katika Boti maalum na Viongozi mbali mbali wa CCM wakielekea Kisiwani Tumbatu Zanzibar kwa ajili ya ufunguzi wa Maulid ya kuadhimisha Sherehe ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W),ikiwa ni sehemu ya ziara yake aliyoanza jana Unguja.
MUFTI Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi , akisoma dua katika Maulid ya kuadhimisha Sherehe ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) Kisiwani Tumbatu.
********************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru Ally Kakurwa,amesema Viongozi na Waumini wa Dini mbali mbali wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Nasaha hiyo ameitoa katika Maulid ya kuadhimisha sherehe ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) huko katika Msikiti wa Gomani kisiwani Tumbatu,Maulid hayo ambayo ni makubwa katika kisiwa hicho yaliyofanyika Novemba 26 ya mwaka 2019 sawa na mwezi 28 mfungo sita 1441 Hijjiria.
Dkt.Bashiru alieleza kuwa japokuwa Serikali haina dini haiimanishi dini haina mchango katika maendeleo ya nchi,na kinyume chake taasisi hizo za kiimani zina mchango mkubwa katika maendeleo unaotakiwa kulindwa na kuenziwa kwa gharama yoyote.
Alisema kinachozuiwa ni tabia za kuendekeza imani kali za kidini zinazosababisha madhara ya kuchonganisha,kubaguana na kufarakanisha jamii na kusababisha machafuko na migogoro ya kuharibu Amani ya nchi.
“Miiko ya muumini yeyote ndio Miiko ya raia mwema yoyote,Masharti ya dini yoyote ndio masharti ya Serikali yoyote yenye ustawi wa maendeleo.
Tuna kila sababu ya kulinda tunu hii ya Amani na Utulivu wa nchi ambayo msingi wake ni uwezo wa uhuru wa kuabudu bila mipaka, na kila Mwananchi kuheshimu dini ya mwenzake.’,alisema Dkt.Bashiru.
Aliwakumbusha Waumini wa dini hiyo kila wanapokutana wakumbushane historia ya uhuru wa Dini uliopo hivi sasa nchini.
Aliongeza kuwa Amani na Utulivu wa nchi havikupatikana hivi hivi bali bali umetokana na juhudi za Serikali zote mbili ya Tanzania bara na Zanzibar, zilizofanya kazi ya ziada ya uwepo wa misingi hiyo.
Alisema viongozi wa dini wanaoelekea katika uzeeni na wale waliofariki wanatakiwa kila Maulid kukumbukwa mchango wao walioutoa katika huduma za kiimani kwani wao ni alama tosha ya kupanda mbegu bora ya kiimani kwa watoto na vijana wa kiislamu.
Pia Katibu Mkuu huyo Dkt.Bashiru, akitoa nasaha zake, alisema daima Waumini wa dini hiyo wathamini na kuenzi juhudi za Waasisi Taifa ambao ni Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Karume na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwani ndio waliopigania uwepo wa haki ya uhuru wa kuabudu.
Katika maelezo yake Dkt.Bashiru, aliwataka Vijana wa Tumbatu kulinda Historia iliyotukuka ya Maulid hayo ya kiimani na kijamii ili yaendelee kufanyika kwa ufanisi kwa kila mwaka.
Kupitia maulid hayo Dkt.Bashiru,aliwasihi Wazazi,Walezi na Viongozi mbali mbali wa Dini na Serikali kuwa karibu zaidi na Walimu wa Madrasa kwa kuwatimizia mahitaji yao ya msingi ili wanaendee kufundisha watoto kwa bidii kwani wengi wanajitolea.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu, Mhe.Haji Omar Kheri aliwashukuru Wageni waalikwa kwa kuthamini hafla hiyo ya Maulid kwani ushiriki wao ni sehemu ya Umoja na Mshikamano wa Waumini wa Dini ya Kiislamu nchini.
Mhe.Haji,alisema msikiti huo wa Gomani yanapofanyika maulid una historia kubwa ya harakati za Ukombozi na Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964, kwani Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Karume aliwasihi kufika katika Msikiti huo katika harakati za kufanya Mapinduzi ya kuondosha dhiki na dhuruma kwa Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar.
Mapema Maelfu ya Waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kwa ujumla walijitokeza katika bandari ya Tumbatu, kumpokea Katibu Mkuu wa CCM Dkt.Bashiru Ally aliyekuwa mgeni rasmi, ambaye yupo nchini kwa ajili ya siku ya ziara ya siku tisa (9) ya kikazi ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi.