Home Mchanganyiko UMMY:SERIKALI HAITAVUMILIA UKATILI WA KIJINSIA NCHINI

UMMY:SERIKALI HAITAVUMILIA UKATILI WA KIJINSIA NCHINI

0

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu akizungumza chimbuko wa siku 16 za Kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia katika uzinduzi uliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Wanawake (UN-Women) Hodan Addou akieleza mchango wa shirika hilo katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa  kijinsia wakati wa uzinduzi wa siku 16 za Kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) Anna Meela Kulaya akieleza jinsia Shirika lake linavyoshirikiana na Serikali katika kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili katika uzinduzi wa siku 16 za Kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Baadhi ya wanafunzi kutoka Shule za Sekondari za Mkoa wa Dodoma wakiwa katika uzinduzi wa siku 16 za Kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Msanii Barbabas Classic akitumbuiza katika uzinduzi Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja wanafunzi wa moja ya shule ya Sekondari ya Dodoma mara baada ya uzinduzi wa siku 16 za Kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

…………….
Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Afya Maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto,Ummy Mwalimu amesema serikali ya awamu ya tano haiwezi kuvumilia vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuwa vinaathiri maendeleo ya Taifa.

Ummy ametoa kauli hiyo leo katika uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, jijini hapa.

Amesema serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na vitendo hivyo kwa kutumia sheria zilizopo.

Waziri Ummy, amesema serikali imekuwa ikitumia gharama nyingi katika kushughulikia waathirika wa vitendo vya ukatili ambapo fedha hizo zingeweza kutumika katika kutoa huduma nyingine za kijamii.

“Kwa mujibu wa benki ya Dunia baadhi ya nchi hutumia hadi asilimia 3.5 ya pato ghafi la taifa kugharamia ukatili wa kijinsia, serikali ya awamu ya tano haiwezi kuvumilia vitendo hivi kwa kuwa vinaathiri maendeleo,”alisema.

Ameagiza walimu wakuu wa shule msingi na sekondari nchini kutoa idadi ya mimba kila baada ya miezi mitatu.

“Kuwepo kwa ukatili wa kijinsia hapa nchini kunachangia Taifa kutofikia uchumi wa kati wa Viwanda kwa sababu nguvu kazi nyingi inapotea kwa kutofikia malengo yao,”amesema.

Aidha, ametoa wito kwa wadau kutumia kampeni hiyo kufanya tathmini maeneo yote yanayohusiana na vitendo vya ubakaji ili kubainisha kiwango cha tatizo hilo na kupendekeza mikakati ya kushughulikia suala hilo.

Awali, Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika(WiLDAF), Anna Kulaya, ameomba serikali kutunga sheria maalum inayoshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia na mahakama ya familia ili kuharakisha kesi za ubakaji ambazo zimekuwa zikikwama kwa kukosa ushahidi.

“Kwa mujibu wa taarifa ya uhalifu wa kibinadamu iliyotolewa na jeshi la polisi kwa mwaka 2018, inaonesha kati ya matukio 11,759, matukio ya ubakaji yalikuwa ni 7,617 sawa na asilimia 64.7,”amesema

Amesema kumekuwapo na mitazamo tofauti kwa jamii hasa ya kutoa taarifa na ushahidi pale matukio ya ubakaji yanapotokea kutokana na wanaofanya vitendo hivyo ni watu wa karibu na wakuaminika.

Naye, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN-Women), Hodan Addou, amesema mwanamke mmoja kati ya watatu duniani wanafanyiwa ukatili wa kijinsia.

“Inakadiriwa wasichana milioni 15 duniani wamekumbana na vitendo vya ubakaji huku kwa Tanzania asilimia 17 ya watu wamefanyiwa ukatili wa kijinsia,”amesema.

Amesema vitendo vya ubakaji kwa tafiti mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika vinashamiri na kugharimu fedha nyingi.

“Ukiweza kuzuia kila ubakaji wowote zaidi ya Dola za Kimarekani 122,000 huokolewa na katika nchi nyingi za Afrika zaidi ya nusu ya gharama za ubakaji hulipwa kupitia vyanzo vya mapato vya serikali ikiwemo Afya, Huduma za jamii, na mfumo wa mahakama nchini,”amesema.

Amesema serikali ikiwekeza katika kuzuia vitendo hivyo itaimarisha hali ya afya na maisha bora kwa wanawake na watoto na hatimaye kuokoa maisha yao.