Watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wametakiwa kuendelea kufanya kazi kama familia moja, huku wakiendelea kudumisha upendo, Amani na mshikamano miongoni mwao hatua itakayowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Wito huo umetolewa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe.Gabriel Malata wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika mkutano uliofanyika leo ndani ya ukumbi wa ofisi hiyo uliopo jijini Dar es Salaam.
Mhe. Malata ameeleza kuwa upendo, amani na mshikamano baina ya watumishi hao ndio chachu ya maendeleo katika ofisi, Kwani upendo ukidumu utapelekea watumishi kushirikiana kwa karibu zaidi.
‘Sisi bado ni familia ndogo sana, hivyo ndugu zangu nawaomba tuendelee kupendana, kusaidiana na kudumisha mawsiliano ya karibu baina ya watumishi vilevile kama kuna kitu haupendi kutendewa usimtendee mwenzako, alisema Mhe. Malata.
Mhe. Malata pia amewataka mawakili hao kwenda mahakani bila kujali idara wanazotoka ili waweze kuwa mahili katika kuendesha mashauri ya aina zote yaani yale ya madai na usuluhishi kwani ili uwe mwanasheria mzuri lazima uwe bora katika kuendesha kila aina ya shauri.
Akizunguza kuhusu kuwapa uzoefu mawakili wachanga Mhe. Malata amewataka mawakili wenye uzoefu kuendelea kuwasimamia mawakili wachanga hasa pale wanapoenda kwenye mashauri makubwa ili waweze kuwapa uzoefu wa namna ya kushughulikia mashauri hayo.
Kiongozi huyo pia amewataka mawakili hao kuwa tayari kuisemea na kuitetea serikali wakati wote wanapotakiwa kufanya hivyo, kwani hiyo ndio sifa halisi ya wakili wa serikali, huku akisisitiza kuwa kila wakili ahakikishe anakuwa bora katika kuendesha mashauri ya aina zote badala ya kujikita na mashauri yanayoihusu idara yake tu.
Aidha Mhe. Malata amesisitiza kuwa ni mhimu kuwapa ushirikiano mawakili wenzetu hasa wale wa mikoani kwani kwa kufanya hivyo itawaongezea morali ya kufanya kazi hatua itakayosaidia kuweza kujenga timu moja ambayo ni imara kwa manufaa ya taifa.
Akisisitiza umhimu wa kuwahi kazini kiongozi huyo mwandamizi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali amewataka watumishi hao kuacha mara moja tabia ya kuchelewa kufika kazini sambasamba na utoro hasa pale viongoji waandamizi wanapokuwa safarini.
Kupitia mkutano huo Mhe. Malata amewashukuru watumishi wote wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kumpa katika kutekeleza majukumu yao huku akiwataka kuendelea kuwa wavumilivu wakati huu ambapo yeye na viongozi wenzake wanapoendelea kushughulikia changamoto mbalimbali za kitumishi katika kuhakikisha wanaweka mazingira bora na rafiki kwa watumishi wote.