Afisa wa Jeshi la Polisi ,ASP Fatuma Mtambo akitoa mada kuhusu ukatili wa kijinsia kwa wafanyakazi wa kiwanda cha Tanzania Distilleries Limited (TDL) cha jijini Dar es Salaam jana ikiwa ni maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo kampuni ya TBL Group inashiriki katika kampeni za kutokomeza vitendo hivyo.
Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL), kwa mara nyingine mwaka huu inaungana na mashirika yanayopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi- Kitengo cha Dawati la Jinsia katika kituo cha Chang’ombe jijini Dar es Salaam na Kisarawe mkoani Pwani.
Maadhimisho haya huandaliwa kila mwaka na Shirika lisilo la kiserikali la WiLDAF kwa kushirikiana na mtandao wa mashirika yanayopinga ukatili wa kijinsia nchini (MKUKI), wadau wa maendeleo na taasisi mbalimbali za kiserikali na za binafsi.
Mwaka huu maadhimisho haya yamelenga zaidi kupinga vitendo vya ubakaji na kuelimisha jamii ya watanzania juu ya athari za ukatili wa kingono na kuhimiza kila mmoja wetu kubadili fikra zetu, kuvunja ukimya na kuchukua hatua juu ya vitendo vya ukatili huo.
Meneja Mawasiliano wa TBL, Abigail Mutaboyerwa, alisema mwaka jana TBL ilitumia maadhimisho haya kwa kuendesha kampeni yake inayolenga kuleta mabadiliko kwenye jamii iitwayo “#IsiweSababu” (#NoExcuse) kuelimisha jamii kuhusu unywaji wa kiustaarabu na kutokutumia pombe kama sababu ya unanyanyasaji wa kijinsia.
Mwaka huu TBL itatumia njia mbalimbali kutoa elimu ya uelewa kwa jamii ikiwemo kuendesha semina kwa wafanyakazi wake na jamii katika maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha Dawati. Vile vile wafanyakazi wa kampuni ya TBL wataungana na Polisi pamoja na wadau mbalimbali kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aliongeza kusema kuwa kampeni hii ya #IsiweSababu itaendelea kutoa elimu mbalimbali ikiwemo kuhimiza jamii kuchukua hatua na kuvunja ukimya na pale pombe kutumiwa kama sababu moja wapo za vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na sababu zingine zinazotumika kulaumu vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake, vitendo vya ukatili dhidi ya wanaume pamoja na watoto hasa watoto wa kike.
Alisema mbali na kujua jukumu la kampuni katika kuelimisha jamii kuhusu unywaji wa kistaarabu TBL ina sera inayohamasisha unywaji wa pombe kwa kistaarabu ili kuepusha madhara mbalimbali ya unywaji wa pombe kupita kiasi ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia.