Baadhi ya Wakuu wa vyuo vya Afya vilivyo chini ya wizara wakifuatilia maelekezo kutoka kwa Katibu mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula (hayupo kwenye picha)wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wakuu wa vyuo vya Afya 37 vilivyo chini ya wizara ya Afya.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akifungua Mkutano wa wakuu wa vyuo vya Afya 37 vilivyo chini ya wizara hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtumba, Jijini Dodoma.
Prof. Andrea Pembe, wakwanza kushoto akiwa na baadhi ya Wakuu wa vyuo vya Afya na baadhi ya Viongozi katika Sekta ya Afya wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wakuu wa vyuo vya Afya 37 vilivyo chini ya Wizara ya Afya, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtumba, Jijini Dodoma.
Wakuu wa Vyuo vya Afya 37 pamoja na baadhi ya viongozi katika Sekta ya Afya, wakifuatilia taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, wakati wa mkutano wa wakuu wa vyuo vya Afya uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtumba, Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasilimali watu Dkt. Saitore Laizer (wakulia) akiwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango Edward Mbanga katika mkutano wa wakuu wa vyuo vya Afya 37 vilivyo chini ya wizara hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtumba, Jijini Dodoma.
**************************************
Na WAMJW-DOM
Katibu mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula amefumua mfumo wa uongozi katika vyuo vya Afya nchini na kuunganisha vyuo vyote vilivyokaribu na hivyo kufanya vyuo kupungua idadi kutoka vyuo 37 hadi kufikia vyuo 9, hali itayosaidia matumizi mazuri ya rasilimali chache zilizopo katika kuzalisha rasilimali watu.
Hayo yamejiri wakati wa mkutano wa wakuu wa vyuo vya Afya 37 vilivyo chini ya wizara hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtumba, Jijini Dodoma.
“Wizara imeona ili kuboresha utoaji taaluma katika vyuo vyake ni vyema kubadilisha mfumo uliopo wa kuendesha vyuo vidogovidogo na kutengeneza mazingira ya kuwa na vyuo vikubwa vichache vyenye mfumo mzuri wa kiuongozi ili kuzalisha Wataalamu sahihi”, alisema.
Dkt. Chaula amesema kuwa, lengo la mkutano huo ni kupanga jinsi ya kuboresha taaluma ndani ya vyuo vya Afya nchini ili kutoa Watumishi bora zaidi jambo litakalosaidia kupunguza vifo visivyokuwa vya lazima kwa kiasi kikubwa.
Mbali na hayo Dkt. Chaula amesema kuwa, mfumo bora wa utawala vyuoni ni muhimili mkubwa na wa msingi katika kuhakikisha mafunzo bora yanatolewa katika vyuo vyetu na wahitimu wanaozalishwa kutoka vyuo hivyo wana umahiri unaokusudiwa katika kutoa huduma za Afya kwa wananchi.
Aliendelea kusema, Wizara imekiri kupokea changamoto za uendeshaji wa mafunzo vyuoni, ikiwemo uchache wa watumishi vyuoni, vifaa vya kufundishia, viwango vya ubora wa wahitimu kushuka, huku akisisitiza mabadiliko ya mfumo wa uongozi yatakuwa chachu ya utatuzi wa changamoto hizo.
Mbali na hayo, Dkt. Chaula amewaasa Viongozi wapya kushughulikia changamoto ya malalamiko kutoka kwa wazazi na wanafunzi wanaosoma vyuoni ikiwemo kukosa kwa baadhi ya haki zao, hali iliyopelekea kwa baadhi ya vyuo kupoteza uaminifu kwa wanafunzi na wazazi.
Nae, Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasiliamali Watu Dkt. Saitore Laizer ametoa wito kwa Wakuu wapya wa vyuo hivyo kufanya kazi kwa ushirikiano baina yao, jambo litalosaidia matumizi mazuri ya rasilimali chache zilizopo katika kuzalisha rasilimali watu.