***********************************
NA EMMANUEL MBATILO
WAZIRI wa Maji ,Profesa Makame Mbarawa jana amefungua Mkutano wa siku mbili wa Mawaziri wa Maji kutoka Nchi za Afrika uliolenga kuangalia Mipango mbalimbali ikiwemo kufanya uendelezaji wa sekta ya maji hasa katika maeneo ya maji safi na maji taka.
Akizungumza katika Mkutano huo uliofanyika Jijini Dar es salaam, Prof.Mbarawa alisema kupitia Mkutano huo wataweza kujadili na kuangalia ni jinsi gani wataweza kuongeza fedha kusaidia katika kuendeleza miradi mbalimbali ya maji.
“Tupo hapa kuangalia ni namna gani tutaweza kuongeza fedha ambazo zitasaidia kuendeleza miradi mbalimbali ya maji pamoja na kuonganisha Taasisi ili ziwe moja ili kuweza kuwafikia wananchi kwa urahisi”Alisema Prof. Mbarawa..
Alisisitiza kuwa pia katika Mkutano huo wataweza kuangalia chagamoto katika eneo la maji taka kwani baadhi ya nchi zimekuwa hazina huduma ya maji taka ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanaziboresha.
Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa Maji kwa wananchi imekuwa ni utamaduni wa Mawaziri hao kukutana na huu ni Mkutano wa Tisa ukiwa umejikita katika kuhakikisha wanamaliza changamoto ya maji.
Aliongeza kuwa Mkutano huo ni wa tisa kufanyika na umejikita katika kumaliza chagamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya maji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa maji safi na maji taka kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika(AFDB)Wambui Gichui alisema Benki hiyo inatambua umuhimu maji hivyo wataendelea kudhamini miradi mbalimbali ili kuimarisha huduma ya maji.