Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa (kulia) akikagua jana chemba ya kutolea upepo kwenye eneo la Uchama wilayani Nzega wakati alipopita kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Mkoani Tabora.
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa(katikati) akitoa maelekezo jana kwa Mkandarasi wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Tabora wakati alipopita Wilayani Nzega kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi huo.
Meneja Mradi kutoka WAPCOS Mattewada Manohar(mwenye T shirt )akimuonyesha Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa(kushoto) sehemu ya maungio ya bomba la kupeleka maji Igunga na yale ya kwenda kwenye tenki la Ushirika Nzega wakati alipopita Wilayani Nzega kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Mkoani Tabora.
NA TIGANYA VINCENT
SERIKALI inatarajia kutumia shilingi bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa bomba za maji ya ziwa Victoria kutoka katika tenki la Ushirika lilipo Nzega mjini kwenda Bukene .
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa wakati alipopita Wilayani Nzega kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Mkoani Tabora.
Alisema kuwa tayari fedha za ujenzi wa mradi huo zipo na usanifu wa mradi huo umeshafanyika ambapo utakuwa umbali wa Kilometa 36 kutoka maji yatakapochukuliwa kwenye tenki la maji la Ushirika lilipo Nzega mjini hadi Bukene.
Profesa Mbarawa alisema katika mpango wa awali Bukene haikuwepo kwenye mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ,lakini Serikali imetafuta pesa kwa ajili ya kujenga mradi huo.
Alisema kwa kuwa fedha zipo kazi hiyo itaanza mara moja ambapo kukamilika kwake utasaidia kutatua tatizo la maji katika Vijiji 19 vya Bukene kwa kuwahakikishia wakazi wa eneo hilo wanapata maji safi na salama mapema.
Awali Mhandisi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoani Tabora (TUWASA), Athuman Kilundumya alisema zaidi ya watu 240,000 wanatarajia kunufaika na ongezeko la eneo la utekelezaji wa mradi wa maji kutoka ziwa Victoria katika Wilaya za Igunga, Nzega na Uyui.
Alitaja maeneo ambayo yatanufaika kuwa ni Bukene wilayani Nzega ambapo Vijiji 19 vitapata maji hayo, Nkinga wilayani Igunga vijiji saba na Kigwa wilayani Uyui , vijiji 16 vya Kata za Igalula, Goweko na Kigwa navyo vinatarajia kupata maji hayo.
Kiludumya alisema kuwa utekelezaji wa mradi wa kuleta maji toka Ziwa Victoria huko katika hatua nzuri na ndani ya wiki tatu maji yatakuwa yamefika katika Manispaa ya Tabora.