Na George Binagi-GB Pazzo, Mwanza
Shirika la Under The Same Sun linaloshughulika na utetezi wa haki za watu wenye ualibino Tanzania limetoa mafunzo kwa akina wanawake wenye ualibino pamoja na wanawake wenye watoto walio na ualibino mkoani Mwanza ili kuwajengea uwezo kuhusu hali ya ualibino.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza Novemba 22, 2019 jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Mfuko wa Kanada kwa ajili ya Mipango ya Kijamii (Canadian Fund for Local Initiative- CFLI) unaotekelezwa katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga.
Mratibu wa mradi huo, Grace Wabanhu amesema matarajio baada ya mradi huo wa miezi minne kufikia tamati ni wanawake hao kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu hali ya ualibino na hivyo kuwa na ujasiri wa kuielimisha jamii inayowazunguka ili kuondokana unyanyapaa na ukatili dhidi ya watu wenye ualibino na hatimaye kuleta usawa katika jamii.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualibino (TAS) Mkoa Mwanza, Alfred Kapole amesema akina mama ni jeshi kubwa hivyo baada ya kuelimishwa kupitia mradi huo watakuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu katika jamii kuanzia ngazi ya nyumbani na hatimaye kusambaa hadi vijijini.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo mama mwenye mtoto aliye na ualibino, Shika Madebe kutoka wilayani Misungwi wameahidi kuitumia vyema elimu watakayoipata kwa kuwaelimisha wanajamii wengine ambao bado hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na ualibino na hivyo kuondokana na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ualibino ambao wamekuwa wakiitwa majina mabaya.
Mmoja wa akina mama mwenye mtoto aliye na ualibino akiwa kwenye mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa kwenye picha ya pamoja.