Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi wakikagua Ujenzi wa Makao wakitoka kukagua Mradi wa Makao Makuu ya Polisi wilayani hapo, leo ikiwa ni harakati za kujenga kituo kipya wilayani hapo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu pamoja na viongozi wengine wilayani Ikungi, wakitoka kukagua Mradi wa Makao Makuu ya Polis wilayani hapo(pichani), leo ikiwa ni harakati za kujenga kituo kipya wilayani hapo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (kulia), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,Edward Mpogolo wakiongozana kuingia katika kituo chakavu cha polisi , leo wilayani Ikungi mkoani Singida. Serikali iko mbioni kujenga kituo kipya ikiwa ni moja kati ya hatua ya kuhamisha kituo hicho pichani ambacho ni chakavu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu,akimuongoza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(watatu)kutoka nje ya Kituo cha Polisi Ikungi , leo wilayani Ikungi mkoani Singida. Serikali iko mbioni kujenga kituo kipya ikiwa ni moja kati ya hatua ya kuhamisha kituo hicho pichani ambacho ni chakavu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
………………….
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe Hamad Yusuph Masauni ametimiza ahadi yake ya kutembelea wilaya ya Ikungi ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Polisi cha wilaya hiyo ambacho ujenzi wake ulisimama kwa muda mrefu.
Hatua hiyo ni kutimiza ahadi aliyoitoa kwa mbunge wa Singida Mashariki Mhe Miraji Mtaturu aliyeihoji serikali ni lini itakamilisha ujenzi wa kituo kipya cha polisi wilaya ya Ikungi kilichosimama kwa muda mrefu ikiwa ni juhudi za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.
Akizungumza katika ziara hiyo baada ya kutembelea kituo kinachotumika hivi sasa na jengo linalojengwa, Masauni amemuelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP)Simon Sirro kutuma wataalam mapema kufanya tathimini ya gharama za ujenzi huo ili kituo hicho kikamilishwe mapema na hivyo kuwezesha askari kupata mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
“Leo nimefika hapa nimejionea kweli mazingira hayaridhishi majengo wanayotumia ya zamani yalikuwa maghala tangu enzi za machifu,serikali ilianza ujenzi wa kituo kipya cha makao makuu ya wilaya lakini kwa bahati mbaya ujenzi huo umesimama,natambua kulikuwa na changamoto lakini kama serikali tutachukua hatua za haraka ili angalau liweze kukamilika tuhamishie askari wetu pamoja na mahabusu hapa waweze kufanya kazi zao ,”alisema Masauni .
“Namuelekeza IGP Sirro alete wataalam hapa wafanye tathimini ya aina mbili,moja tathimini ya gharama zote za ujenzi mpaka kukamilika,pili tujue gharama ya kukamilisha sehemu ya jengo hili na watushauri kitaalam kama linaweza kutumika kwa kukamilisha sehemu ya kuanzia ili watu wahamie,”aliongeza Masauni.
Amesema gharama zikishajulikana kuwa ni kiasi gani IGP Sirro ahakikishe anapata hizo fedha ili waweze kukamilisha angalau sehemu ya kwanza ukizingatia majimbo hayo mawili Singida Mashariki na Singida Magharibi yanapiga hatua kwa kasi sana kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa chuo cha Veta,hospitali na hivi karibuni wanatarajia kuwa na mgodi wa dhahabu hali itakayochangia uwepo wa ongezeko la watu na matukio ya kihalifu pia.
Amempongeza Mhe Mtaturu kwa jitihada zake za kuhakikisha anasemea shida za wananchi ambazo nae anaziishi ili serikali izipatie ufumbuzi,”“Niwaambie wananchi hapa mmepata mbunge anayewawakilisha vizuri bungeni kwa masilahi mapana ya wananchi wote,bungeni alihoji lini tutakamilisha kituo hiki,nami niwaahidi kituo kitakamilika mapema,”alisema Masauni .
Amewapongeza askari wa mkoa wa Singida chini ya Kamanda wa Polisi mkoa Sweetbert Njewike kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na changamoto wanazokumbana nazo.
“Niwahakikishie kuwa dhamira ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ni kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ikiwemo vitendea kazi na makazi ya askari,”aliongeza Masauni.
Akizungumza katika ziara hiyo Mhe Mtaturu amemshukuru naibu waziri huyo kwa kutimiza ahadi yake ya kwenda kujionea hali halisi ya kituo cha polisi cha Ikungi.
“Pamoja na shukrani hizo,mhe naibu waziri niseme hapa Ikungi kwenye mgao wa magari makubwa(Ashoke Leyland) hatukupata,hivyo tunaomba utupatie gari ili liwasaidie askari wetu kuweza kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zao,”alitoa ombi Mtaturu.
Awali Mkuu wa Wilaya hiyo Edward Mpogolo amemshukuru Naibu huyo kwa kitendo chake cha haraka cha kujibu na kutekeleza kile alichoahidi bungeni na kutoa shukrani kwa Rais Magufuli kwa kuvilea vyombo vya ulinzi na usalama.
“Sisi wilaya ya Ikungi tuna changamoto kubwa ukizingatia kwa jiografia ya wilaya yetu ni lazima upite Singida mjini ndio uende kwenye tarafa nyingine,na hapa tunaanza kuwa na machimbo ya dhahabu ambayo pia ni sehemu ya changamoto katika uwepo wa wahamiaji lakini unapokuwa na machimbo uhalifu pia unaongezeka,
“Pia kilimo chetu kinakuwa na uchumi wa watu unazidi kuongezeka hivyo kuongezeka kwa uchumi na kuongezeka kwa fedha kwa watu wetu kunasababisha uwepo wa uhalifu hivyo kituo hiki ambacho serikali inakijenga kinatuhakikishia uwepo wa amani katika wilaya yetu na ujio wake umetupa moyo sana kwamba hiki kituo kinaweza kukamilika hivi karibuni,”alisema Mpogolo.
Mkuu huyo amesema tayari wamepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa mahakama ya kisasa ya wilaya ambayo itaanza kujengwa hivi karibuni hivyo uwepo wa mahakama hiyo na kituo unawapa matumaini makubwa sana.