Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima (wa pili kushoto) akiwasili katika kituo cha kuzalisha gesi asilia cha Mnazi Bay mkoani Mtwara kukagua namna wanavyotekeleza sheria ya mazingira ya mwaka 2004.
Meneja wa mradi wa kuchakata gesi wa kampuni ya Maurel and Prol Tanzania katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara akitoa maelezo kwa viongozi waliotembelea mradi huo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Prof. Esnat Chagu na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka wakitembelea mradi wa gesi uliopo Madimba mkoani Mtwara.
******************************
Na Robert Hokororo, Mtwara
Serikali imeelekeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kushawishi
viwanda mbalimbali nchini kutumia gesi asilia inayozalishwa hapa nchini hatua
itakayosaidia kupunguza matumizi ya nishati zinazoharibu mazingira.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa
Sima ametoa maelekezo hayo alipotembelea miradi ya kuchakata gesi katika
maeneo ya Mnazi Bay na Madimba mkoani Mtwara wakati wa ziara ya kukagua
shughuli za mazingira zinavyofanyika katika miradi hiyo.
Sima pamoja na kupongeza miradi ya uzalishaji wa nishati hiyo alisema kuwa
hakuna sababu ya viwanda kuharibu mazingira kwa kutumia nishati kama mafuta ambayo imezoeleweka na badala yake vianze kutumia gesi asilia ambayo ni rafiki wa mazingira.
“Katika ziara hii tumejifunza mambo mengi na hapa tunaona juhudi zinazofanyika kuhakikisha tunapata gesi asilia na tumeambiwa hapa kinazalishwa, kuchakatwa na kusafirishwa kiwango kikubwa cha gesi hivyo Serikali inaelekeza ninyi TPDC (Shirika la Petroli Tanzania) mkae na CTI (Shirikisho la Viwanda) muwashishi kuona sasa namna ya kutumia gesi asilia na kuachana na mafuta kwani yanaharibu mazingira,” alisema.
Aidha, Sima ambaye aliambatana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) alitoa maelekezo kwa kampuni zinazojihusisha na uchakataji
wa gesi asilia kuomba kibali cha viwango cha uchafuzi wa hewa vinavyozalisha
katika shughuli zao za kila siku.
Alifafanua kuwa viwanda hivi vina jukumu la kufuata Sheria ya Mazingara ya
Mwaka 2004 hivyo pamoja na kuishirikisha jamii kujua madhara yanayoweza
kutokea kutokana na nishati hiz lakini pia ni lazima NEMC watambue viwango
vya uchafuzi wa mazingira hususan katika hewa zinazotokana na shughuli za
uckakataji wa gesi.
“Hi sasa dunia inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo
yana athari kubwa kwa mazingira yetu hivyo tunapoanzisha miradi kama hii
lazima tuombe vibali ili tujue standards za pollution tunazozalisha na kama ikizidi utaratibu basi tuanze kulipa tozo kwa mujibu wa taratibu.
“Tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na viwanda hivi vya gesi na
hapa,tunaambiwa kuna visima takriban vitano na vinafanya vizuri ambapo
takriban futi za ujazo zaidi milioni 90 sawa na asilimia 90 ya pure gas
inasambazwa katika maeneo mengine ya nchi na hapa tayari tuna hazina kubwa
ya nishati hii,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka alitaka
viwanda vyote vinavyojishughulisha na shughuli kama hizo za uchakatiji wa gesi
kuwa na mpango wa jinsi wanavyoratibu uchafuzi wa hewa ili kuweza
kukabiliana na changamoto kama hizo katika mazingira.
Pamoja na mambo mengine pia Dkt. Gwamaka alitaka ziungwe mkono juhudi za
uzalishaji wa gesi zinazofanyika katika miradi hii ili kuweza kuhifadhi mazingira
kutokana na kuepukana na ukataji wa miti kwa ajili ya nishati.
Naibu Waziri Sima na NEMC wako katika ziara kwenyue mikoa ya Lindi na
Mtwara kukagua miradi ya visima vya gesi kuona kama inafuata Sheria ya
Mazingira ya mwaka 2004 na namna mabavyo wanatoa elimu kwa wananchi
kuhusu namna ya kuchukua hatua pindi yanapotokea maafa yakiwemo kuvuja
kwa nishati hiyo katika mabomba.