WAKATI Mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ,Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amewaagiza Wasimamizi wa Uchaguzi wote mkoani humo kuhakikisha wanachukua tahadhari kwa kujenga na kuimarisha Vituo vya Kupigia Kura vilivyopo katika maeneo ya wazi kama vile kwenye miti kwa kuweka Maturubai mapema.
Hatua hiyo inalena kuhakikisha kuwa zoezi la upigaji kura la jumapili ijayo ariathiriwa na maji ya mvua.
Mwanri alitoa kauli hiyo jana wakati wa ziara yake na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Uslama ya Mkoa na ile ya Wilaya ya Nzega , Uyui na Igunga wakati wa kukagua maandalizi ya maeneo ya kupigia kura Jumapili ijayo.
Alisema ni vema Vituo ambavyo vimepangwa katika maeneo ya wazi vikajengwa mapema kwa kutumia Maturubai katika eneo ambalo wananchi watakapotumia kupiga kura na eneo ambalo Mawakala wa Vyama vya Siasa watakapokaa.
Mwanri alisema pia lazima kuwepo eneo ambalo wananachi wanaosubiri kupiga kura wanaweza kujihifadhi endapo mvua itanyesha siku ya uchaguzi.
“Pamoja na kuwa Vituo vya wazi havipo katika majengo na kama mnapanga kujenga Mahema basi wekeni mazingira mazuri ya watu wanaokuja kupiga kura ili wawe na uhakika hata kama mvua ikinyesha ghafla , hatanyeshewa na vifaa vya kupiga kura havitaathirika na mvua” alisisitiza.
Alisema sanjari hilo amewataka Wasimamizi hao kuhakikisha kuwa vifaa vyote vya kuendesha zoezi la uchaguzi vinafika mapema katika eneo la tukio ili kuhakikisha zoezi linakwenda kwa kwa wakati uliopangwa na hakuna wananchi watakaokosa kupiga kura kwa sababu ya ukosefu wa vifaa hivyo.
Kwa upande wa Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Rukia Manduta aliwataka Wasimamizi wa Uchaguzi kuhakikisha kuwa maeneo ambayo watajenga na kuweka Maturubai kuwa kwenye miununoko.
Alisema hatua hiyo itazuia kuharibika vifaa ikiwemo karatasi za kupigia kura kutokana na maji ya mvua
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Selemani Sikieti alisema tayari wameshanunua Maturubai kwa ajili ya kutekeleza zoezi hilo na watachukua tahadhari zote ili kufanya zoezi la upigaji kura kukamilika bila vikwazo