***************************
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HAKUNA jambo lolote linaloanza kwa utelezi hapa duniani. Kila kazi ina changamoto na msoto wake. Na katika kupitia changamoto hizo, baadhi yao wanafikia kukata tamaa kabisa, licha ya kuwa na kila kitu kinachoweza kuwapatia mwangaza katika mambo wanayopigania.
Hata katika sanaa ya muziki wa kizazi kipya tunachoshuhudia vijana wengi wakichanua na kujimudu kiuchumi, pia una suluba na changamoto lukuki, msoto mzito unaowakumba wasanii wengi tangu siku walipoamua kujiingiza kwenye tasnia hiyo.
Katika kuangalia vijana hao wanaopitia katika msoto mzito ni Maneno Mohamed ‘Man Mo’. Kijana huyu mwenye uwezo wa juu wa kuimba na kutunga nyimbo za muziki wa kizazi kipya, anapitia katika tanuri la moto, barabara yenye miba mikali kiasi cha kuwahi kukata tamaa ya kuendelea na sanaa yake.
Ndio, hii ni kwa sababu msanii huyo licha ya kuwa kwenye sanaa kwa muda mrefu sasa, lakini mlango wa mafanikio ulionekana kuchelewa kufunguka, licha ya kuwa na kipaji cha uimbaji na utunzi wa nyimbo kali, ukiwamo wimbo wa ‘Nasimama’ ulioimbwa na msanii nyota Judith Wambura ‘Lady JayDee’, ambao uliandikwa na Man Mo.
Katika mazungumzo na Gazeti hili, Man Mo anasema kwamba alianza kujihusisha na muziki tangu alipokuwa mdogo, akimfuatilia mama yake Bi Salama Mussa Kaduga, aliyekuwa anajihusisha na sanaa katika Matukio mbalimbali haswa ya kisiasa, huko kijijini kwao Kimange, mkoani Pwani.
“Muda mwingi nilikuwa namfuatilia mama yangu katika sanaa yake, jambo ambalo lilichochea kwa kiasi kikubwa mimi kupalilia kipaji changu cha kimuziki na kuweka nia kubwa ya kuja kuwa msanii nyota duniani kama wengine.
“Pamoja na mambo mengine, msanii mwingine ambaye kwa namna moja ama nyingine aliendelea kukuza kipaji changu ni Ali Kiba, ambaye muziki wake niliuelewa, haswa nilipofanikiwa kukutana naye katika studio za Sharobaro Records za jijini Dar es Salaam zilizokuja kuvuma kwa kutoa wasanii wengi mahiri, akiwamo Bob Junior, Diamond Platnumz, Shetta, Rich Mavoco na wengineo kibao ambao mara kwa mara walikuwa wakikutana kwenye studio hizo,”Alisema Man Mo.
Msanii huyo mwenye kiu kubwa kisanaa anasema rasmi kuingia kwenye sanaa ilikuwa ni mwaka 2010 ambapo kama vijana wengine, aliamua kuondoka kijijini kwao na kuvamia jiji la Dar es Salaam, akiwa na matarajio makubwa ya kuvuna kwa kupitia muziki wa kizazi kipya.
Kwa bahati mbaya jiji lilimlaki vibaya na kumchoma na jua tangu alipofika na kuamua kukimbilia kwenye kiwanda Cha nguo Cha Urafiki ili apunguze makali ya kimaisha kwa kufanya kibarua katika kitengo cha kuchambua nyuzi. Mkali huyo wa kizazi kipya anasema licha ya kufanya kibarua Urafiki, lakini hamu ya kimuziki ilikuwa kubwa na kujikuta akienda Sharobaro kurekodi wimbo wake kwa pesa yake, hata hivyo baadae uongozi wa Studio hizo ulimpa ahueni kwa kumtaka awe chini ya Sharobaro Records ili akue kimuziki. Hata hivyo anakiri uamuzi huo pia ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na bidii yake pamoja na kujituma kwa kila aina ikiwamo kufanya usafi kwenye studio hizo, akitafuta upenyo wa kuchomoka kisanaa.
“Nikiwa Sharobaro Records nilifanikiwa kurekodi nyimbo nyingi na kupata marafiki wengi ambao naweza kusema nilikua kwa kiasi kikubwa mno kulinganisha na wakati ule natokea kwetu kijijini nikiwa sina mtandao wowote kisanaa na hata kula yangu ikawa ni mashaka matupu.
“Nyimbo ambazo nilitengeneza wakati ule ni Binti wa Kibara, Binti wa Kimasai na nyingine nyingi ambazo hazikuachiwa hewani bila kusahau zile nilizoandikia wasanii wengine ukiwamo ule wa dada yangu Lady JayDee uliojulikana kama Nasimama ambao ulifanya vizuri mno katika ulingo wa Bongo Fleva,”Alisema.
Wakati anaamini anaelekea pazuri, ghafla mambo yalibadilika na kurudi tena kwenye msoto ambapo kila alilopanga lilishindwa kutimia, ikiwamo kuwapata mameneja ambao bila wao ni ngumu msanii kutokea peupe. Anasema wakati anaelekea kuchoka, akapata meneja aliyempa sharti la kuimba muziki wa injili na sio muziki wa kidunia.
“Huyu ndugu yangu alikuwa anaitwa James Albert Katagira anayemiliki shule za Tusiime, ambaye alinionea huruma na msoto wangu na kunishawishi nihamie kwenye injili ili anisimamie jambo ambalo nililitekeleza haraka, kwa sababu lengo langu lilikuwa ni sanaa.
“Nilifanikiwa kurekodi nyimbo mbili na video zake ambazo ni Jicho Langu na Nimuimbie, ambazo zilifanya vizuri katika muziki wa injili na kuanza kupata shoo nyingi katika mikoa mbalimbali kwa kuunganishwa na wasanii wengi wa muziki huo bila kusahau kushiriki makongamano mengi ya kidini,”Alisema.
Man Mo anasema muziki huo ulikuwa unampa mwelekeo mzuri, licha ya kufikia kutengwa na familia yake kwa madai alitokea katika chimbuko la waumini wa dini ya Kiislamu, hivyo jamii ilishindwa kumuelewa, wakiwamo marafiki zake waliomkosoa kwa kitendo chake cha kuacha Bongo Fleva na kukimbilia injili.
Ili jamii imuelewe akiwamo mama yake mzazi, alitumia muda mwingi kuzungumza nao, huku akikiri kuwa aliingia kanisani na kuimba injili kama njia ya kumfikisha kileleni na sio nia ya kubadili dini, ingawa anasema katika kipindi chote hicho, jamii ya kikristo na wasanii hao wameishi kwa upendo na kushirikiana kwa kiasi kikubwa, akiwamo Madame Frola ambaye alishiriki naye katika matamasha kadhaa likiwamo la Tanga Mjini akiwa kama mwimbaji wa injili.
Man Mo anasema msoto haukumuacha, kwani msaada wake uligota, hivyo kuamua kuachana kabisa na muziki, akiingia katika biashara ya kilimo pamoja na kuuza kuku, biashara ambazo zilitokana na umri kuendelea kumtupa mkono huku akishindwa kutokea peupe.
Kijana huyo mwenye ndoto na maneno mengi mdomoni mwake anasema baada ya kukaa kwa miezi kadhaa bila kujihusisha na lolote linalohusu muziki, alishtushwa na simu kutoka kwa Belo Master, aliyekuwa anafanya wimbo kwenye Studio za classic Sound chini ya mtayarishaji wake Monagenster za Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
“Wakati ananipigia simu, sikuwa na ari, lakini kwakuwa jamaa anajua uwezo wangu na alitaka nikamuimbie kiitikio, hivyo nikaenda Studio kurekodi kama alivyotaka, jambo ambalo lilianza upya kunitekenya rohoni mwangu.
“Kwakuwa niliimba vizuri kwenye wimbo ule, viongozi wa Monagenster walivutiwa na mimi na kunivuta karibu ili waendelee kuangalia uwezo wangu ambapo walinikubali zaidi haswa kwa uwezo wangu wa kuandika nyimbo kali, ukizingatia wengi nilikuwa nawatungia, hivyo kupata upenyo rasmi,”Alisema.
Kijana huyo anasema kwa Sasa anasimamiwa kazi zake chini ya Kampuni ya African Network Entertainment (ANE) kwa kushirikiana na Monagenster kwa kupitia classic Sound ambapo hadi sasa nimeachia nyimbo mbili kali pamoja na video matata ambazo ni ‘Tike na Mapenzi Kazi zinazofanya vizuri katika ulimwengu wa muziki.
Msanii huyo anayetokea kwenye familia ya watoto wanne, huku yeye akiwa wa kwanza kuzaliwa mwaka 1994 huko Kimange, anawataja wadogo zake kuwa ni Mwahija, Sauda na Muhsin huku kiwango chake cha elimu kikiwa ni kidato cha nne, akiishia kiwango hicho kutokana na kuhangaikia muziki licha ya baba yake kutamani mtoto wake asome sana, aliishia njiani.
Man Mo alisoma elimu ya msingi katika shule mbili za Kimange na Bagamoyo, wakati elimu ya Sekondari aliipata katika shule ya Air wing ya Banana, jijini Dar es Salaam, huku akisema kuwa maisha ya muziki kabla ya kutoka ni magumu yanayoweza kukatisha tamaa wasanii wengi wenye vipaji.
“Kwa sasa sina ninachokifanya zaidi ya kusikiliza ushauri wa viongozi wangu wa ANE, nikiamini kuwa uwezekano wa kupasua anga ni mkubwa kutokana na Kampuni kuwa na watu wanaojua muziki na ndoto za sisi vijana kufika mbali.
“Lengo langu ni kufanya muziki mzuri wa kibiashara, nikitumia uzoefu wangu na kipaji changu cha kuimba na kuandika nyimbo kali ili nipate mafanikio ya kutimiza ndoto zangu, ukizingatia kuwa nimesota sana, nimekula ngarambe nyingi, hivyo hakuna kinachoweza kuniweka chini tena,”Alisema Man Mo.
Man Mo anasema kuwa licha ya muziki kuwa na ushindani mkubwa, lakini ukiweka bidii unafanikiwa, huku akisema kuwa anataka kuwa msanii ‘simple’ kama Ali Kiba lakini afanye muziki mzuri wa biashara kama Diamond Platnumz jambo linalompa utajiri mkubwa.
Msanii huyo anaendelea kusema kwa kuwataka wasanii kufanya juhudi kubwa kuutangaza muziki wao pamoja na chipukizi kukaza msuri ili nao wafikie malengo licha ya kwamba wasanii wachanga wengi huishia njiani kwa kushindwa kwenda na kasi ya msoto katika sanaa.
Man Mo anakumbuka jinsi alivyoshindwa kuwa na maelewano mazuri na baba yake kiasi cha kununiana, kisa kuwa kwenye muziki huku maisha yakiwa magumu kwa mtoto wao, ambapo juhudi za mama yake zilikuwa zinamlainisha mzee wake japo kwa uchache.
Mwimbaji huyo mwenye ndoto kubwa anasema muziki umezidi kupiga hatua kutokana na juhudi za wasanii wenyewe wanaokwenda na mabadiliko, ikiwamo mbinu ya kutumia vizuri mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, YouTube nk, ambapo kama ilivyokuwa kwa wasanii wengine, Man Mo pia anamiliki akaunti mbalimbali zinaoenda kwa jina la manmoofficial katika mitandao mbalimbali kwa ajili ya kutangaza muziki wake pamoja na kupata ulingo wa kujadiliana na mashabiki wake.
Anasema hali hiyo umeufanya muziki kuwa biashara nzuri licha ya msoto kabla ya kutoka kuwa pale pale, jambo linaloongeza hamasa ya kufanya vizuri kwa wasanii wote nchini Tanzania, ambapo nyimbo zake zinapatikana kwenye YouTube kwa akaunti ya Kampuni ya Africa Network Entertainment pamoja na kupatikana pia Audiomack, Boomplay, Spotify na kwingineko.
Kuhusu serikali, Man Mo anaitaka iendelee kushirikiana na wasanii wote sanjari na kuwatafutia upenyo katika muziki wa Dunia, bila kusahau kufanikisha wasanii wa ndani kutoka nje mara kwa mara ili wakaongeze wigo mkubwa katika sanaa yao, akisisitiza kuwa bila wasanii wa ndani kupata maonyesho ya Kimataifa muziki wao hautapiga hatua.