Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi wakikagua Ujenzi wa Makao wakitoka kukagua Mradi wa Makao Makuu ya Polisi wilayani hapo, leo ikiwa ni harakati za kujenga kituo kipya wilayani hapo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu pamoja na viongozi wengine wilayani Ikungi, wakitoka kukagua Mradi wa Makao Makuu ya Polis wilayani hapo(pichani), leo ikiwa ni harakati za kujenga kituo kipya wilayani hapo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (kulia), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,Edward Mpogolo wakiongozana kuingia katika kituo chakavu cha polisi , leo wilayani Ikungi mkoani Singida. Serikali iko mbioni kujenga kituo kipya ikiwa ni moja kati ya hatua ya kuhamisha kituo hicho pichani ambacho ni chakavu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu,akimuongoza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(watatu)kutoka nje ya Kituo cha Polisi Ikungi , leo wilayani Ikungi mkoani Singida. Serikali iko mbioni kujenga kituo kipya ikiwa ni moja kati ya hatua ya kuhamisha kituo hicho pichani ambacho ni chakavu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
******************************************
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kutuma timu ya wataalamu kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kufika wilayani Ikungi Mkoani Singida, kutathmini maendeleo ya Ujenzi wa Ofisi na Kituo kipya cha Polisi baada ya kituo cha awali kuchakaa hali inayopelekea askari na mahabusu kukaa sehemu isiyo salama.
Ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya kutembelea Wilayani Ikungi ikiwa ni kuitikia wito wa Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, aliyetaka kauli ya Serikali juu ya uchakavu wa Ofisi, kituo cha polisi Ikungi na hali mbaya ya chumba cha mahabusu wakati wa kipindi cha maswali katika kikao cha Bunge kilichoisha hivi karibuni.
“Nimefika hapa nimeona mazingira wanayofanyia kazi hayaridhishi, serikali ilishaanza Ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya lakini ujenzi umesimama kwa miaka mitano sasa, namuagiza IGP Sirro alete wataalamu waje wafanye tathmini juu ya gharama za umalizwaji ujenzi huu na baada ya kujua basi hatua za haraka zifanyike ili ujenzi huu ukamilike” alisema Masauni
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu amesema hali ya kituo cha polisi hicho ni mbaya huku mahabusu wakikaa sehemu chafu ambayo si salama kwa afya ya binadamu.
“Mheshimiwa Naibu Waziri kama nilivyokueleza bungeni wakati nikiuliza swali la nyongeza nadhani sasa umejionea hali ilivyo mbaya, humo ndani umesikia harufu katika chumba cha mahabusu,wanajisaidia humo lakini pia umeona askari wanavyofanya kazi kwenye mazingira mabovu, naomba sasa serikali muangalie uwezekano wa kuharakisha kituo kile kipya hata mkianza na sehemu tu itasaidia adha hii wanayopata wananchi wa wilaya hii” alisema Mbunge Mtaturu.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogoro amesema uwepo wa kituo hicho kipya kikikamilika kitaimarisha Ulinzi na Usalama wilayani hapo ambapo kumekua na changamoto za kiusalama kwasababu ya upya wa wilaya hiyo ambayo imeanza.