Wasichana watano kutoka Mkoa wa Singida, waliochaguliwa kushiriki mashindano ya mbio za wanawake (Ladies First) 2019 wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutangazwa Kwenye eneo la viwanja vya michezo Shule ya Sekondari ya Mwenge mjini hapa leo. Kutoka kulia ni Emmy Hosea, Zakia Said, Faidha Ally, Tunu Andrea na Elvera Emmanuel.
Afisa Michezo na Utamaduni wa Mkoa wa Singida, Henry Kappela akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani), wakati akiwatangaza wanariadha wateule.
Washiriki wa mashindano hayo ngazi ya mkoa wakisikiliza hotuba za viongozi wao.
Afisa Michezo na Utamaduni wa Wilaya ya Ikungi, Abubakari Kisuda, akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mashindano hayo ngazi ya mkoa.
Maofisa Michezo wa Mkoa wa Singida wakiwa kwenye shughuli hiyo. Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Chama cha Riadha, Said Swalehe, Katibu wa Chama cha Riadha, Juma Mataka na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Riadha, Juma Jambau.
Wanariadha hao wakionesha mshikamano.
Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Singida, Benno Msanga (wa tatu kutoka kuli), akiwa na Wanariadha hao.
Wanariadha hao wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi.
Na Waandishi Wetu, Singida
Washiriki watano wa mchezo wa riadha kwa wasichana kutoka Shule mbalimbali za mkoa wa Singida wamechaguliwa kushiriki mashindano ya “Ladies First ” 2019 kitaifa yanayotarajiwa kufanyika mwezi ujao jijini Dar-es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mashindano ya ‘Ladies First’ ngazi ya mkoa, Afisa Utamaduni na Michezo Mkoa wa Singida, Henry Kapella alisema wanariadha
wateule wanatarajia kuungana na wezao kote nchini mapema kuanzia Disemba 7-8 mwaka huu.
Aliwataja washindi hao na maeneo wanayotoka kuwa ni Emmy Hosea (Itigi) ambaye atakuwa na kibarua cha kushiriki mbio za mita 100 na mita 200, Zakia Said (Manyoni)atakimbia mbio za mita 400 na 800,Faidha Ally (Ikungi) atakimbia mita 1500, Tunu Andrea (Ikungi) mita 500, pamoja na Elivila Emanuel (Ikungi) mita 1500.
“Lengo la mashindano haya ni kumwezesha mtoto wa kike kushiriki kikamilifu katika michezo hususani mchezo wa riadha,” alisema Kapella.
Kapella alisisitiza kuwa mara baada ya kumalizika kwa mashindano hayo ngazi ya Taifa washindi watapata nafasi ya kushiriki mashindano hayo ngazi ya kimataifa yatakayofanyika Septemba 2020 nchini Japan.
Kapella alisema mashindano hayo ngazi ya mkoa yamewezeshwa na kuratibiwa na Katibu Tawala wa Mkoa huku ngazi ya kitaifa yakitarajiwa kudhaminiwa na Baraza la Michezo la Taifa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).