***************************************
Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
iliwasilisha ombi la kupatiwa fedha toka Mfuko wa Kimataifa wa Kukabiliana na
Mabadiliko ya Tabianchi -Green Climate Fund (GCF) ili kutekeleza mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Mkoa wa Simiyu ikiwa ni mkakati wa Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi (Simiyu Climate Resilient Water Supply Project).
Mradi huu utatekelezwa katika wilaya tano za Mkoa wa Simiyu ambazo ni Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu na utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu utajumuisha wilaya za Busega, Itilima na Bariadi kwa muda wa miaka mitano na kuwanufaisha wananchi 858,959. Gharama za mradi zitachangiwa kwa pamoja kutoka Serikali ya Tanzania na Wadau wa Maendeleo.
kulingana na Mkataba wa Makubaliano ya Utoaji Fedha -Financing Agreement (GCF) watachangia EURO Milioni 102.7, Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la Benki ya Maendeleo ya Ujerumani itachangia EURO Millioni 26.1 na Serikali ya Tanzania EURO Millioni 40.7 na Wananchi kupitia nguvu zao (In kind Contribution) watachangia EURO Millioni 1.5. Aidha, mradi huu utakuwa maeneo makuu manne ya utekelezaji ambayo ni; uboreshaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira, uanzishaji wa kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi (Climate Smart Agriculture), ujenzi wa mabwawa madogo madogo ya umwagiliaji na kujenga uwezo katika usimamiaji wa mradi. Serikali imeanza taratibu za kufanya uthamini wa mali na ardhi kwa wananchi wote
watakaotakiwa kupisha ujenzi wa miundombinu ya mradi itakayojumuisha ujenzi wa njia ya bomba kuu la maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Miji ya Wilaya za Busega, Bariadi na Itilima lenye urefu wa kilometa 167.
Kwa kuwa gharama za utekelezaji wa mradi unajumuisha ufadhili kutoka taasisi za kimataifa, taarifa ni muhimu kuwajulisha wananchi kabla ya kuanza rasmi zoezi la uthamini.
Uthamini utafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999, Sheria ya Uthamini Na.7 ya Mwaka 2016 na Sheria ya Utwaaji wa Ardhi Na. 47 ya Mwaka 1967 pamoja na miongozo yake.
Kwa taarifa hii Serikali inawajulisha wananchi wote ambao maeneo yao yatapitiwa na mradi kuwa, kazi ya uhamasishaji na hatimaye uthamini itaanza kuanzia tarehe 27 Novemba, 2019.