Msimamizi wa Miradi wa taasisi ya TCRS mkoa wa Morogoro,Rehema Samweli, akizungumza na wakulima wa kijiji cha Diovuva, kata ya Kiloka, Halmashauri ya Morogoro vijiji.
Baadhi ya wakulima wakimsikiliza kwa makini Msimamizi wa Miradi wa taasisi ya TCRS, mkutano uliolenga kubaini changamoto zinazowakabili na kutafuta nmana ya kuwaunganisha na masoko ya mijini.
……………..
NA VICTOR MAKINDA. MOROGRORO
Wakulima wa mboga mboga na matunda wa kijiji cha Diovuva kata ya Kiloka, Halmashauri ya Morogoro vijijini wamesema kuwa wanakabiliwa na changamoto lukuki zinazo kwamisha juhudi zao za kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya kilimo, sekta inayoajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania.
Wakizungumza katika mkutano wa wakulima hao uliondaliwa na Taasisi ya kuwahudumia wakimbizi ya Tanganyika (TCRS), mkutano uliolenga kuzibaini changamoto za wakulima hao na kutafuta namna ya kuzitatua, wakulima hao walisema kuwa ukosefu wa soko la uhakika, bei duni ya mazao sambamba na ujazo mkubwa maarufu kama rumbesa ni miongoni mwa changamoto zinazo wakabili.
“ Sisi wakulima wa mboga mboga na matunda wa kijijini hapa tunakabiliwa na changamoto nyingi. Kubwa ni kukosa soko la uhakika la kuuza mazao yetu. Kijiji hiki hakina soko. Lipo gulio tu ambalo hufanya kazi mara mbili kwa wiki. Kama ujuavyo baadhi ya mazao tunayozalisha huoza haraka. Tunaposubiri siku mbili kwa wiki kwa ajili ya kuuza mazao hayo kwenye gulio hutusababishai hasara ya kuoza au tunauza kwa bei ya chini kwa kuhofu kuwa hakuna mahali na siku nyingine tunawez kuuza. Alisema Siraji Rajabu mkulima wa Nyanya kijijini hapo.
Siraji aliongeza kusema kuwa ukosefu wa barabara ya uhakika ya kusafirishia mazao yao ni kikwazo kingine kinachowafanya kuuza mazao yao kwa bei ya chini hali inayowasababishia hasara.
Naye Kudra Jumanne mkulima wa mboga mboga wa kijijini hapo alisema kuwa ukosefu wa huduma za ugani ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili na kupelekea kuzalisha kwa hasara kwa kuwa mazao yao hushambuliwa na wadudu.
“ Sijui kama tunaye afisa ugani hapa kijiji kwetu. Hatumjui na hatijawahi kupata huduma zake. Tunalima kienyeji tu, hatujui namna sahihi ya kutumia mbegu, madawa ya kuulia wadudu na mbole. Mazao yetu yanashambuliwa sana na wadudu.Hatujui nani tumweleze kwa kuwa ukimtafuta mtaalamu wa kilimo kwa ajili ya kupata maelezo ya kitaalamu hapatikani. Alisema Kudra.
Naye Imani Idy mkulima wa vitunguu saumu na tangawizi kijiji hapo alilalamikia ujazo mkubwa wa mazao maarufu kama lumbesa kuwa ni kikwazo kwa ukuaji wa uchumi wao.
“Wanapokuja wanunuzi siku ya gulio, ni tatizo kubwa. Hawataki ujazo wa kawaida. Kinyume chake wanatutaka wakulima kujaza lumbesa. Lumbesa inatufanya kuuza mazao mengi kwa bei ndogo ambayo haifanani na gharama za uzalishaji. Tunashangaa serikali ya kijiji na kata wamekaa kimya kuhusu kadhia hizi ambazo wakulima tunazipata. Alisema Imani.
Akizungumzia changamoto hizo, Diwani wa kata ya Kiloka, Jamila Taji, alisema kuwa ni kweli wananchi wa kijiji hicho wanakabiliwa na changoto ya barabara ya Kiloka Diovuva, ambayo haipitiki hasa masika, ukosefu wa soko la kijiji. Yeye kama diwani amekuwa akisisitiza masuala hayo katika vikao ya Halmashauri kwa kipindi kirefu na kwa sasa mipango ya ujenzi wa soko na barabara hiyo ipo mbioni.
“ Kuhusu huduma za ugani yupo mtaalamu wa kilimo wa kata, lakini hakuna wa kijiji. Labda wakulima hawamtumii lakini yupo na ninaahidi kumsukuma aende kwa wananchi kuwahudumia. Na hili la ujazo wa lumbesa nitamwelekeza mtendaji kufuatilia. Alisema Taji.
Msimamizi wa miradi wa shirika la TCRS mkoani Morogoro, Rehema Samweli akieleza madhumuni ya mkutano huo, alisema kuwa shirika lake limedhamiria kuwasaidia wakulima wa kijiji hicho kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo changamoto ya masoko kwa kuwaunganisha na wafanyabisahara wa mijini ili wawe na uhakika wa kuuza mazao yao kwa kwa bei yenye tija.