Mtakwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Kitengo cha Takwimu za makosa ya Jinai madai na jinsia Asha Mussa Mahfoudh akitoa takwimu za makosa ya barabarani ambapo imeonekanwa kupanda kutoka ajali 22 kwa mwezi wa Oktoba 2018 hadi ajali 32 kwa mwezi wa Oktoba 2019, hafla iliyofanyika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa habari waliohudhuria katika Mkutano kuhusiana na utoaji wa takwimu za ajali ambapo imeonekanwa kupanda kutoka ajali 22 kwa mwezi wa Oktoba 2018 hadi ajali 32 kwa mwezi wa Oktoba 2019.
Mkuu wa Kitengo cha takwimu za uhalifu makao makuu ya Polisi Zanzibar Ispekta Khamis Mwinyi Bakari (katikati) akijibu maswali yaliyoulizwa na Waandishi katika mkutano wa utoaji wa takwimu za makosa ya ajali za Barabarani ambapo imeonekana kupanda kutoka ajali 22 kwa mwezi wa Oktoba 2018 hadi ajali 32 kwa mwezi wa Oktoba 2019 sawa na asilimia 45 .5, hafla iliyofanyika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar.
Picha na Yussuf Simai – Maelezo Zanzibar.
………………………………………..
Na Mwashungi Tahir,Maelezo
Jumla ya makosa 2,032 ya makosa ya barabarani pamoja na ukiukwaji wa sheria yameripotiwa katika vituo mbali mbali vya polisi kwa mwezi wa Oktoba 2019 mwaka huu.
Hayo aliyasema Mtakwimu Mkuu wa Serikali kwenye kitengo cha takwimu za makosa ya Jinai ,Madai na jinsia Asha Mussa Mahfoudh wakati akizungumza na waandishi wa habari huko katika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Mazizini .
Amesema idadi ya ajali barabarani kwa mwaka uliopita zimeongezeka kutoka ajali 22 kwa mwezi wa Oktoba , 2018 hadi 32 mwezi wa Oktoba , 2019 sawa na 45.5.
Akizungumza kuhusu ajali za barabarani Afisa huyo amesema jumla ya ajali 32 zimeripotiwa kutokea mwezi wa Oktoba mwaka huu ambapo waliofariki ni 19 na waliojeruhiwa ni 33.
Kwa upande wa ukiukwaji wa sheria wa makosa ya barabarani , Magharibi A na Magharibi B zimeongoza zaidi kwa makosa ya kushindwa kuvaa sare na beji kwa Tingo na Madereva wa gari za abiria, kutofuata miongozo na kanuni za usalama barabarani.
Alisema makosa mengine ni kuendesha vyombo vya moto ikiwemo gari,vespa,pikipiki na fifti bila ya leseni wala bima na kukosa kuvaa helmet pamoja na kuzidisha idadi ya abiria na mizigo.
Nae Inspekta Khamis Mwinyi Bakari kutoka Kitengo cha Takwimu za uhalifu kutoka Makao Makuu ya Polisi amewataka madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani ili kupunguza ajali kutokana na ubovu wa barabara .
Kwa upande wa Koplo Khamis Juma kutoka Ofisi ya Mkuu wa kikosi cha usalama wa barabarani amesema ongezeko la ajali barabarani katika Wilaya ya Magharibi A linatokana na ubovu wa barabara ikiwemo njia ya Bububu kwa kisasi na mshelishelini hivyo amewataka madereva kuwa waangalifu ili waweze kupungua ajali za kizembe