Home Mchanganyiko WAFANYABIASHARA ARUSHA WAPEWA SIKU MOJA KUHAMISHIA SHUGHULI ZAO NDANI YA SOKO

WAFANYABIASHARA ARUSHA WAPEWA SIKU MOJA KUHAMISHIA SHUGHULI ZAO NDANI YA SOKO

0

*********************************

Na Tito Mselem Arusha,

Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa siku moja kwa Wafanyabiashara
wote wa Madini Mkoani Arusha kuhamishia shughuli zao ndani ya Soko
na watakao bainika kununua madini nje ya Soko watachukuliwa hatua
za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni zao na kufikishwa Mahakamani.

Hatua hiyo inafuatia ziara ya kushtukiza ya Waziri Biteko aliyoifanya
Sokoni hapo Novemba 13, 2019 na kubaini changamoto za wanunuzi
Wakubwa wa Madini kutolitumia Soko hilo na badala yake wameendelea
kununua Madini nje ya Soko.

Katika zira yake hiyo, Waziri Biteko ameambatana na viongozi
mbalimbaliwa Serikali pamoja na Wizara ya Madini akiwemo Katibu
Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume
ya Madini Prof. Idris Kikula, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Mkoa wa Arusha
Jonathan Shanna na wengine.

Pia, Waziri Biteko amemtaka Mkandarasi anayeendelea na ujenzi katika
Soko hilo ahakikishe anamalizia haraka ujenzi huo huku
wafanyabiashara wakiwa wanaendelea na shughuli zao katika Soko hilo.
Aidha, Waziri Biteko amemuagiza Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof.
Idris Kikula kumuondoa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Robert
Erick kwa kushindwa kusimamia ipasavyo shughuli za Madini Mkoani
humo.

Afisa Madini huyo anadaiwa kuwaachia wafanyabiashara wakubwa wa
Madini Mkoani Arusha kufanya biashara ya Madini maofisini mwao
tofauti na maelekezo ya Serikali iliyowataka wafanye biashara hiyo
kwenye Masoko ya Madini ambapo ofisi nne tu ndizo zilikuwa wazi
wakati Soko hilo lina ofisi za wafanyabiashara wakubwa 40 lakini kwa
zaidi ya miezi minne hawajahamia katika ofisi hizo.

Alisema jukumu hilo la kusimamia kufanya biashara ndani ya Soko hilo
na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wenye madini majumbani
mwao ni jukumu la Afisa Madini, lakini kazi hiyo kwa sasa inafanywa na
Waziri hatua ambayo haikubaliki kabisa, wakati wa kulindana umepitwa
na wakati sio kwa Serikali hii iliyopo madarakani.

Waziri Biteko alisema kuwa, biashara ya Madini ya Tanzanite Mkoani
Arusha imeshuka kwa asilimia kubwa na wanaofanya biashara hiyo
wanajulikana  lakini hawachukuliwi hatua  na kwamba ofisi yake haiko
tayari kuona ubadhilifu wa aina hiyo.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Biteko amesema kuwa haoni
sababu za msingi za wafanyabiashara wakubwa wa Madini Mkoani
Arusha kushindwa kufanya biashara katika Soko la Madini lililoandaliwa
na Serikali na badala yake wafanyabiashara hao wanafanya biashara
katika ofisi zao.

Amewaeleza wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo wa Madini Mkoani
Arusha kuwa haitaji kupigiwa makofi kwani yeye anasimamia kanuni na
sheria namba 20 ya Madini inayosema kuwa kila mfanyabiashara wa
Madini awe Mdogo ama Mkubwa anapaswa kufanya biashara ndani ya
Soko la Madini na sio vinginevyo.

Ameongeza kuwa, Wafanyabiashara wakubwa waliomba muda wa
mwezi mmoja katika kufanya biashara ndani ya Soko hilo na Wizara
iliongeza muda huo waliohitaji lakini hadi sasa ni zaidi ya miezi minne
hakuna mfanyabiashara mkubwa aliyekuwa akifanya bishara katika
Soko hilo na badala yake wanafanya biashara katika ofisi zao na
wanamiliki kilo nyingi za madini kinyume cha utaratibu.

Waziri amesema anazo taarifa za uhakika baadhi ya wafanyabiashara
wakubwa 97 wana ofisi za madini Arusha na Nairobi na wanafanya
ujanja ujanja ili wafanye biashara hiyo kwa njia haramu na kuikosesha
Serikali mapato hilo halikubaliki watachukuliwa hatua kali ikiwemo
kufilisiwa mali zao na kufikishwa Mahakamani.

Akizungumzia suala la wafanyabishara Wadogo wa Madini amesema
ofisi yake ina idadi ya wafanyabishara wenye leseni  263 lakini
wanaofanya biashara hiyo mtaani ni zaidi ya watu 1,300 hali inaonesha
wazi kuwa  zaidi ya wafanyabiashara 1037 wanafanya biashara bila ya
kuwa na leseni na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha analijuwa hilo
lakini ameshindwa kusimamia majukumu yake ya kazi.

Pamoja na mambo mengine Waziri Biteko amesisitiza uaminifu katika
sekta ya madini.