Home Mchanganyiko MKURUGENZI WA HUDUMA ZA TUME YA MADINI AFANYA ZIARA MTWARA

MKURUGENZI WA HUDUMA ZA TUME YA MADINI AFANYA ZIARA MTWARA

0

Mkurugenzi wa Huduma za Tume ya Madini, William Mtinya (kulia) akipokelewa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Ephrahim Mushi (kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi hiyo iliyopo mjini Mtwara Mkoani Mtwara ikiwa ni sehemu ya ziara yake yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ofisi hiyo tarehe 14 Novemba, 2019.

Mkurugenzi wa Huduma za Tume ya Madini, William Mtinya (katikati) akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara

Mkurugenzi wa Huduma za Tume ya Madini, William Mtinya (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara

************************************

Na Greyson Mwase, Mtwara

Leo tarehe 14 Novemba, 2019 Mkurugenzi wa Huduma za Tume ya Madini, William Mtinya amefanya ziara katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Ephrahim Mushi ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara yenye lengo la kujifunza na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wanaofanya kazi katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi katika mikoa husika.

Katika ziara yake, Mtinya aliambatana na Afisa Utumishi wa Tume ya Madini, Jeremiah Chuma pamoja na Meneja Habari na Mawasiliano wa Tume ya Madini, Greyson Mwase.

Mara baada ya kuwasili na kupokelewa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Ephrahim Mushi pamoja na watumishi na kuelezwa changamoto mbalimbali zinazoikabili ofisi husika, Mtinya aliwataka maafisa madini wakazi wa mikoa nchini kufanya kazi kwa kujiamini huku wakifuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.

“Napenda mtambue jukumu kubwa mlilopewa katika usimamizi wa Sekta ya Madini katika kuhakikisha inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa pato la Taifa; kwa mfano katika mwaka wa fedha 2019-2020 tumepangiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 470, ni vyema mkaweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mnasimamia vizuri shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na ukusanyaji wa kodi mbalimbali,” alisema Mtinya.

Mtinya alishauri maafisa madini wakazi wa mikoa kujenga mtandao kwa ajili ya
kubadilishana uzoefu pamoja na kushauriana mambo mbalimbali ya kikazi na
kuendelea kusisitiza kuwa, Tume ya Madini Makao Makuu ipo tayari kupokea na
kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zitakazowasilishwa.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtinya alielekeza maafisa madini wakazi wa mikoa kuchambua pamoja na kuainisha orodha ya leseni ambazo hazifanyiwi kazi ili uandaliwe utaratibu wa kuziandikia hati ya makosa kabla ya kufutwa rasmi.

Aliendelea kusema kuwa, ni vyema leseni husika wakapewa wachimbaji wenye nia ya kuendesha shughuli za madini badala ya kukaa nazo tu huku Serikali ikipoteza mapato yake.

Akielezea mikakati ya Tume ya Madini katika kuhakikisha inavuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019-2020, Mtinya alieleza kuwa ni pamoja na kutoa ajira mpya 166 kwa kada mbalimbali ambapo wataalam watasambazwa kwenye ofisi za maafisa madini wakazi wa mikoa nchi nzima na kwenye masoko ya madini.

Aliendelea kufafanua kuwa, ofisi zenye upungufu wa watumishi zitapewa kipaumbele lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wadau wa madini nchini.

Alieleza kuwa hatua nyingine zilizofanywa na Tume ya Madini ni pamoja na ununuzi wa magari 36 ambapo mpaka sasa magari 12 yemeshapokelewa na kusisitiza kuwa juhudi zinaendelea kufanywa ili kuhakikisha Desemba mwaka huu, magari yote yatakuwa yameshapokelewa.

Aliendelea kusema mbali na upatikanaji wa magari, pia Tume ya Madini imepata
maderava wapya 20 ambao wametawanywa katika mikoa mbalimbali ya kimadini.

Aliongeza kuwa, Tume ya Madini imeshaagiza vifaa mbalimbali vya kupima madini vitakavyotumika kwenye masoko ya madini, lengo likiwa ni kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki.

Katika hatua nyingine, Mtinya aliwapongeza watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara kwa kufanya kazi kwa weledi na uzalendo mkubwa na kuwataka kuendelea kuchapa kazi kwa bidii huku Ofisi ya Makao Makuu ya Tume ya Madini ikiangalia namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Wakati huohuo, wakizungumza katika nyakati tofauti watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara waliupongeza Uongozi wa Tume ya Madini kwa kufanya ziara katika mkoa wa Mtwara na kuahidi kuongeza ubunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli na kufikia lengo lililokusudiwa.

Awali watumishi hao waliwasilisha changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kutosha kwenye shughuli za upimaji wa madini, magari ya ziada kwa ajili ya kufuatilia maeneo ya mbali yenye shughuli za madini, upungufu wa watumishi wa kada ya jemolojia n.k