Mtaalam wa ulinzi na usalama wa mtoto kutoka UNICEF Bi. Victoria Mgonela akiongea na washiriki wa mkutano wa Jukwaa la Haki Mtoto.
Washiriki wa Mkutano wa Jukwaa la Haki Mtoto wakisikiliza mada kutoka kwa mwezeshaji
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi na washiriki wa Mkutano wa Jukwaa la Haki Mtoto.
Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Patience Ntwina akifungua mkutano wa siku mbili wa Jukwaa la Haki Mtoto unaopitia na kuboresha rasimu ya mkakati wa pili wa miaka mitano wa Haki mtoto unaoendelea Jijini Dodoma.
***************************
“Wizara ya Katiba na Sheria imejidhatiti katika kuhakikisha masuala ya Haki
yanasimamiwa kwa umakini ili kila mmoja wetu aweze kufurahia uhuru, amani na utulivu pasipo kuvunja sheria za nchi.”
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki Bw. Patience Ntwina wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Haki Mtoto kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria. Mkutano huo wa siku mbili unaoendelea Jijini Dodoma umekutanisha wadau mbalimbali ukiwa na lengo la kupitia na kuboresha rasimu ya Mkakati wa Pili wa Miaka Mitano wa Haki Mtoto.
Bw. Ntwina alisema Katika kutimiza hayo, Wizara ya Katiba na Sheria imekuwa
ikisimamia mifumo ya haki na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na bila
upendeleo wala uonevu wa aina yoyote.
Alisema “ mifumo ya haki inawaangalia watu wote bila kujali hali ya mtu. Na hii ndio ilipelekea Wizara ya Katiba na Sheria kuja na mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria na sheria zingine kama Sheria ya kuwalinda watoa taarifa na sheria ya upashaji wa habari. Hii yote ni kuhakikisha Haki inapatikana kwa wakati na kwa watu wote”.
Aliongeza, masuala ya watoto ni mtambuka katika Wizara na sekta mbalimbali na hivyo utekelezaji wake unahitaji mpango mkakati mahususi ili kuwezesha kila mdau kutekeleza majukumu yake katika maeneo yaliyobainishwa ili kupata ufanisi na tija katika kumhudumia mtoto.
Mpango Mkakati wa Pili wa Haki Mtoto unategemea kuangalia kwa kina na kukidhi matakwa yaliyopo kwenye mazingira ya sasa na kukamilisha yale ambayo hayakutekelezwa kwenye mkakati wa kwanza ambao uliisha mwaka 2017.
Aidha alitoa shukrani kwa washirika wa maendeleo ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuendesha Mpango Mkakati wa Haki za Watoto na shughuli za Jukwaa la Haki Mtoto.