Muuguzi kutoka Hospitali ya Mloganzila, Bw. Mosama John akiwaelekeza
wataalam namna ya kuwahudumia wateja wanaokuja hospitalini hapa.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Njoikiki
Mapunda wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila akizungumza wakati wa
kufunga mafunzo elekezi kwa wataalam tarajali 80 ambapo amewataka kufanyia
kazi yote waliyofundishwa ili kuwa watumishi bora.
Mtaalam elekezi wa masuala ya Ukimwi kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti
Ukimwi (TACAIDS), Bw. Patrick Kanyamwege akiwaelimisha wataalam tarajali
kuhusu maambukizi ya Ukimwi na jinsi ya kujikinga.
Waaalam Tarajali wakifuatilia mada mbalimbali zinazowasilishwa katika
mafunzo elekezi katika Hospitali ya MNH-Mloganzila.
Afisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) Bi. Heavenlight Majule akiwasilisha mada kuhusu udhibiti wa
rushwa mahala pa kazi.
****************************
Watoa huduma wa afya wameaswa kuzingatia uadilifu na uaminifu mahala pa kazi kwa kutokuomba wala kupokea rushwa wakati wa kutoa huduma.
Hayo yamezungumzwa na Afisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati wa kufunga mafunzo elekezi kwa
wataalam tarajali 80 walioko kwenye mafunzo ya mwaka mmoja katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa njia ya vitendo yanayolenga kuwawezesha
kutoa huduma bora za afya kwa jamii.
“Kupokea zawadi au pesa kabla na baada ya kutoa huduma ni kosa kisheria na
pindi utakapogundulika umefanya hivyo basi utachukuliwa hatua kulingana na
vifungu 24 vya makosa ya rushwa vilivyoainishwa katika sheria namba 11 ya
mwaka 2007 ya kuzuia na kupambana na rushwa,” Amesema Bi. Majule.
Amesisitiza kila mmoja ana wajibu wakushiriki katika mapambano dhidi ya
rushwa kwa kutoa huduma bora za afya bila malipo yoyote kwani rushwa
humnyima haki anayepatiwa huduma na kupunguza ufanisi katika kazi.
Kwa upande wake Muuguzi katika Hospitali ya Mloganzila, Bw. Mosama John
ametoa wito kwa wataalam hao kuwa na kauli nzuri wakati wa kuwahudumia
wateja wanaokuja hospitalini hapa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Mada ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na elimu elekezi juu ya
udhibiti wa rushwa mahala pa kazi, elimu ya maambukizi ya ukimwi na jinsi ya
kujikinga, kanuni za maadili ya utendaji kwa watumishi wa Umma, matumizi bora ya vifaa tiba na dawa, huduma za kliniki, mahusiano kwa Umma na huduma kwa wateja.