Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mohamed Mtanda kitabu kinachoonyesha Mpango wa ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Tanzania alipofika ofisini kwake kumtembelea akiwa katika ziara ya kikazi mkoa wa Rukwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Nkasi alipomtembelea Mkuu wa wilaya hiyo ofisini kwake akiwa katika ziara ya kikazi mkoa wa Rukwa.
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Nkasi wakimsikiliza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa wilaya ya Nkasi waliofika Mahakamani kupata huduma za kimahakama.
Lydia Churi Ntambi
…………………….
Na Lydia Churi-Mahakama Rukwa
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu nchini kuanza kuzipitia Sheria na kanuni zinazohusu uchaguzi ili kujiandaa kusikiliza kesi za uchaguzi.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Nkasi wakiwemo Mahakimu, Jaji Mkuu amewataka Mahakimu kuanza kujiandaa kusikiliza kesi za uchaguzi kwa kuwa mwaka huu nchi itafanya uchaguzi wa Serikali za mitaana baadaye mwakani uchaguzi mkuu.
Aidha, Jaji Mkuu pia ameagiza Mahakimu kutochelewesha kesi za uchaguzi kwani alisema kwa kufanya hivyo wataweza kuiingiza Mahakama kwenye migogoro. Aliongeza kuwa endapo kesi hizo zitasikilizwa kwa mujibu wa sheria na kumalizika kwa wakati zitasaidia kuifanya Mahakama kuendelea kuaminiwa zaidi na wananchi.
Alisema endapo Mahakimu watazipitia sheria na kujiandaa vema kusilikilza kesi hizo kni wazi kuwa hawatababaishwa mahakamani. “Hakimu anayefahamu sheria na taratibu hawezi kubabaishwa awapo Mahakamani”, alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu pia amewataka Mahakimu kutojihusisha na masuala ya siasa ili waweze kuwa huru katika kutatua migogoro mbalimbali itakayoletwa kwao. Alifafanua kuwa Sheria inamkataza Jaji, Msajili, na Hakimu kujiunga na chama chochote cha siasa ili waweze kutatua migogoro inayoletwa kwao.
Awali akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Nkasi, Said Mohamed Mtanda, Jaji Mkuu amesema Mahakama ya Tanzania inao mpango wa kuwa na mahakama za Mwanzo za kisasa kwenye kwenye kila tarafa kwa nchi nzima ili kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi.
“Tutahakikisha tunajenga Majengo ya kisasa ili endapo tarafa husika itakuwa wilaya basi majengo hayo yawe na hadhi ya kuwa Mahakama za wilaya”, alisema Jaji Mkuu. Alisema Mahakama itaiomba Serikali Kuu kupeleka fedha za ujenzi wa majengo hayo kwenye halmashauri ili halmashauri zijenge.
“Sisi tutatoa ramani za majengo, tutatafuta na fedha ili halmashauri zijenge kwa kuwa tayari zinao uzoefu katika kujenga vituo vya afya hivyo na jukumu la kujenga Mahakama za Mwanzo mlibebe.”
Awali akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Nkasi, Said Mohamed Mtanda alipomtembelea ofisini kwake, Prof. Juma alihimiza ushirikiano wa Mahakama na mihimili mingine kwa kuwa Katiba ya nchi pia inatambua na imegawa majukumu kwa kila mhimili ambapo mihimili yote humtumikia mwananchi.
Naye Mkuu wa wilaya ya Nkasi, Said Mohamed Mtanda amesema Serikali wilayani humo itashirikiana na Mahakama ya Tanzania kwa karibu ili kuhakikisha wananchi wa wilaya hiyo wanapata huduma zote muhimu zikiwezo huduma za mahakama.
Jaji Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Rukwa ambapo leo alitembelea Mahakama za wilaya ya Nkasi na Namtumbo.