Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof.Ibrahim Hamis Juma,akisalimiana na watumishi wa mahakama ya wilaya ya Kalambo mara baada ya kuwasili kukagua shughuli za mahakama akiwa katika ziara ya kikazi Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga Mkoani Rukwa.
……………………
Na Lydia Churi-Mahakama Rukwa
Benki ya Dunia imeipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kutekeleza vizuri mradi wa maboresho ya huduma za mahakama kupitia Mpango mkakati wake wa miaka mitano (2015/16-2016/2019).
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliwasilisha pongezi hizo kutoka Benki ya Dunia kwa watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kalambo alipokuwa akizungumza nao akiwa katika ziara ya kikazi kukagua shughuli za Mahakama mkoani Rukwa.
Alisema taarifa ya ukaguzi iliyoandaliwa na ujumbe wa Benki ya Dunia uliofika nchini Februari 4 hadi 15, 2019 kufanya ukaguzi imetoa pongezi hizo kufuatia Mahakama kuzipitia sheria na kanuni zaidi ya 50 na kuzifanyia marekebisho ili kurahisisha utoaji wa haki nchini.
Jaji Mkuu aliyataja maeneo mengine yaliyopongezwa na Benki ya Dunia kuwa ni hatua iliyochukuliwa na Mahakama ya kutunga kanuni mpya zinazoongoza Madalali wa pamoja na zile zinazoongoza Mawakili.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, maeneo mengine ni matumizi sahihi ya mfumo wa taarifa za kusajili mashauri (JSDS II), kwa kuwa katika mfumo huo hakuna taarifa chafu iliyowahi kuingizwa na kila shauri linalosajiliwa huingizwa kwenye mfumo siku hiyo hiyo linaposajiliwa.
Aidha, Benki ya Dunia imeisifu na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kujiwekea malengo na kufanya kazi inayoonyesha matokeo na kujiwekea viwango au mikakati ya kupunguza mashauri ya mlundikano. Benki hiyo pia imeipongeza Mahakama kwa aina ya ujenzi wa majengo ya mahakama kwa kuwa yanazingatia kukua kwa matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Maeneo mengine yaliyoonyesha mafanikio na kupongezwa na Benki ya Dunia ni kitendo cha Mahakama kujiwajibisha yenyewe katika utendaji kazi wake hasa kwa kujiwekea mifumo ya kujiwajibisha na kufanyiwa tathmini ya utendaji wake na Taasisi inayojishughulisha na masuala ya utafiti ya Repoa.
Kufuatia pongezi hizo, Jaji Mkuu amewataka watumishi wa Mahakama kuendelea kutambua nafasi pekee ya Mahakama katika jamii kwa kuwa Mahakama hutoa uamuzi kwa kuzingatia taratibu ilizojiwekea.