Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Rahabu Kibona (kulia) akiwakabidhi Namba za Utambulisho kwa Mlipakodi (TIN) mara baada ya kusajiliwa wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa Mikoa ya Morogoro na Pwani.
Afisa Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Julius Mjenga akiwaelimisha Wafanyabiashara wa Ifakara mjini mkoani Morogoro wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa Mikoa ya Morogoro na Pwani.
Afisa TEHAMA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Shukuru Bathoromeo akimsajili Mfanyabiashara wa Rupiro mkoani Morogoro wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa Mikoa ya Morogoro na Pwani.
(PICHA ZOTE NA TRA)
****************************
Na Veronica Kazimoto
Ifakara
Wafanyabiashara wa Ifakara Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wameelimishwa kuhusu Kodi ya Zuio katika eneo la ukodishaji majengo na ardhi ambapo mpangaji anapaswa kukata kodi na kuwasilisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) asilimia kumi ya kiasi cha malipo walichokubaliana katika mkataba wa upangishaji.
Akizungumza wakati wa Kampeni ya Usajili, Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayofanyika mkoani Morogoro, Afisa Kodi Mkuu, Julius Mjenga amewataka wapangishaji kutowazuia wapangaji kukata asilimia 10 ya malipo ya mkataba kwakuwa kodi hiyo inatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato na inasimamiwa na TRA.
“Kodi ya zuio inatozwa kwa mujibu wa sheria na anayeisimamia sheria hiyo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania hivyo wapangishaji wote mnapaswa kutowazuia wateja wenu ambao ni wapangaji wa majengo na ardhi kuwasilisha asilimia kumi ya malipo kufuatana na mkataba mlioingia,” alisisitiza Mjenga.
Mjenga ameeleza kuwa, kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wapangishaji kuwakatalia wapangaji wao kukata asilimia hiyo na pale wapangaji wanapolazimisha husitishiwa mkataba au kupewa notisi ya siku 90.
“Iwapo mpangishaji atakaidi malipo hayo ya asilimia kumi yasikatwe na mpangaji kwa lengo la kuyawasilisha TRA, mpangishaji huyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015,” alisema Mjenga.
Kodi ya zuio inatozwa katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na malipo ya mishahara, mirabaha, hisa, upangishaji na gawio mbalimbali ambapo kila eneo limepangiwa kiwango cha asilimia kinachotakiwa kulipwa.
Kampeni ya usajili, huduma na elimu kwa mlipakodi imeanza tarehe 11 na itamalizika tarehe 17 Novemba, 2019 na inafanyika katika wilaya zote za Mikoa ya Morogoro na Pwani.