Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu Bi Emmy Hudson (aliyesimama) kutoka RITA akizungumza na Waandishi wa Habari akitoa maelekezo ya mgogoro wa ITOA.Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi Sheria RITA Lina Msanga
Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu Bi Emmy Hudson kutoka RITA akitoa Taarifa ya Uchunguzi wa Mgogoro wa Bodi ya Wadhamini Wakulima wa Chai Igominyi -Igominyi Tea Out grawers Association(ITOA)
Mkuu wa Wilaya ya Njombe (wa pili kulia)akiwa pamoja na Ujumbe kutoka Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu RITA na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
………………
HYASINTA KISSIMA,AFISA HABARI-HALMASHAURI YA MJI NJOMBE
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umetoa hatma ya Mgogoro uliokuwa ukihusisha Bodi ya Wadhamini wa Chai Igominyi –Igominyi Tea Out grawers Association (ITOA) mara baada ya Ofisi ya Kabidhi Wasihi Mkuu inayosimamia bodi za wadhamini kufanya uchunguzi na kubaini uwepo wa migogoro katika suala la udhamini na utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa mazao ya Kimkakati yanakuwa chini ya ushirika na sio bodi za wadhamini, na kusabisha hekta 357.3 zilizokuwa zinamilikiwa na ITOA kukabidhiwa Halmashauri ya Mji Njombe.
Akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Emmy Hudson amesema kuwa Uchunguzi uliofanywa na timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Msajili Vyama vya Hiari, Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu Ofisi ya Mrajisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri imebaini kukiukwa kwa taratibu kwa mujibu wa sheria zilizowamilikisha maeneo hayo.
“Lengo la mashamba waliyokabidhiwa ITOA ilikuwa ni kwa lengo la kuyaendeleza kupitia kilimo mkakati. Timu ya uchunguzi imebaini kuwa mashamba hayo hayakutumika kama yalivyokusudiwa. Yapo pia maelekezo ya Serikali yaliyotoewa kuwa Taasisi zote zinazojishughulisha na mazao ya kimkakati ikiwemo chai ziweze kujisajili kwenye vyama vya ushirika. Ofisi yangu imeelekeza kwamba mashamba hayo yarejeshwe kwenye Halmashauri ili iweze kupanga matumizi ambayo yatajielekeza katika kuendeleza zao la chai ambalo ni zao la Kimkakati.”Alisema Emmy
Aidha Bi Emmy amesema kuwa yapo mambo ambayo kwa kushirikiana na taasisi yake yanatakiwa kutekelezwa ndani ya siku thelathini ili kufanikisha maelekezo yaliyotolewa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri alisema kuwa mgogoro wa ITOA ni miongoni mwa changamoto zilizokuwa zinakabili wakulima wa chai kwa muda mrefu na amepongeza kwa jitihada zilizochukuliwa kwani kwa sasa Mashamba hayo yatakuwa chini ya Mkurugenzi na wakulima wa chai kuendelea kunufaika na kuishukuru RITA kwa maamuzi yaliyofikiwa.