Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya Sala ya Ijumaa, kwenye Msikiti wa Nunge, Jijini Dodoma, Novemba 8, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisikiliza mawaidha, kabla ya Sala ya Ijumaa, kwenye Msikiti wa Nunge, Jijini Dodoma, Novemba 8, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Alhaji, Ismail Dawood, baada ya Sala ya Ijumaa, kwenye Msikiti wa Nunge, Jijini Dodoma, Novemba 8, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia mkono wananchi, wakati akitoka kwenye Msikiti wa Nunge, Jijini Dodoma, Novemba 8, 2019, baada ya kushiriki sala ya ijumaa.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kudumisha amani na utulivu uliopo nchini kwa kuishi kwa umoja na upendo ili kujiletea maendeleo kuanzia mtu binafsi hadi jamii nzima kwa ujumla.
Ametoa wito huo leo (Ijumaa, Novemba 08, 2019) wakati akitoa salamu kwa waumini wa dini ya kiislam aliposhiriki sala ya Ijumaa kwenye msikiti wa Nunge Jijini Dodoma.
“Waislam wenzangu pamoja na jamii nzima hatuna budi kuendelea kutunza amani iliyopo kwa maombi hasa kuwaombea viongozi wetu wa kitaifa kuongoza nchi kwa hekima na busara katika kuimarisha umoja na upendo uliopo nchini.”
Waziri Mkuu alieleza kuwa, ni muhimu kutambua mchango wa dini katika Taifa kwa kuzingatia kuwa ndicho chombo chenye nguvu kuleta misingi mema kupitia mawaidha na mafundisho yanatolewa kwa makundi yote hususan kundi la vijana ambalo linategemewa katika nguvu kazi ya Taifa.
Aliongezea kuwa, dini zina mchango mkubwa katika kuimarisha uwepo wa amani ambayo inatoa fursa kwa jamii kushiriki vema kwenye shughuli za uzalishaji mali za kila siku, hivyo jamii haina budi kuzingatia yale wanayofundishwa katika dini zao ili kudumisha umoja, mshikamano na upendo.
“Tuendelee kuungana pamoja bila kujali tofauti za imani zetu na hii itasaidia kuwa na maendeleo endelevu na kuendelea kuwaombea viongozi wote nchini wawe na afya njema.”
Aidha pamoja na hayo aliliasa kundi la vijana ambalo ni nguvu kazi ya Taifa liendelee kutumia nafasi zao katika kujishughulisha kwa bidii katika kazi za uzalishaji na kuondokana na makundi yasiyofaa.
Kwa upande wake, Mtoa mawaidha katika ibada hiyo Ustadh Omari alimshukuru Mhe.Waziri Mkuu na akatumia nafasi hiyo kuwakumbusha Watanzania waendelee kufanya kazi kwa bidii na jitihada ili kuondokana na magenge ya mitaani yanayoshiriki katika mambo maovu ikiwemo uhalifu unaohatarisha amani na utulivu.
“Vijana lazima mfanye kazi kwa bidii na kuendelea kumtumikia Mungu anayewapa uhai bila kusahau ibada na hii itasaidia kuondokana na makundi ya machokoraa ambao tunaamini wangejifunza masuala ya elimu ya Mungu ingewasaidia na kuwa na Taifa lenye viongozi wazuri wa kesho” alisisitiza Ustadhi Salim.
Waziri Mkuu alisema anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za Maulid ya kuzaliwa Mtume (S.A.W) kwa niaba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli zitakazofanyika Kitaifa Mkoani Mwanza tarehe 09 Novemba, 2019.
Aidha kwa mkoa wa Dodoma wanatarajia kuadhimisha kwa kuwa na maandamano yatakayoanzia katika viwanja vya Nyerere Squere hadi msikiti wa Mkuu wa Gadaff.