Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene akizungumza wakati wa kikao cha kupokea tathmini ya uharibifu wa uoto wa asili iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine.
Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akitoa maelezo kuhusu tathmini ya uharibifu wa uoto wa asili iliyofanywa katika Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni agizo la Makamu wa Rais. Mhe. Samia Suluhu Hassan
Mkuu wa Kitengo cha Mifumo ya Kijiografia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Benedict Mugambi akiwasilisha maelezo ya kazi iliyofanyika katika Mkoa wa Shinyanga ya upimaji uoto wa asili na ukusanyaji takwimu mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene pamoja na wajumbe.
Sehemu ya wajumbe kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakifuatilia kikao cha kupokea taarifa ya kazi ya ukusanyaji takwimu na upimaji wa uoto wa asili iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mkoani Shinyanga.
Wajumbe kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakifuatilia kikao cha kupokea taarifa ya kazi ya ukusanyaji takwimu na upimaji wa uoto wa asili iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mkoani Shinyanga.
……………………
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene amesema ipo haja ya kufanya kongamano la taifa la mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambalo litawahusisha wadau ili kuboresha sekta hiyo.
Simbachawene amesema hayo wakati akipokea taarifa ya tathmini ya uharibifu wa uoto wa asili iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika maeneo ya Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni maagizo ya Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan alipofanyika ziara mkoani humo mwanzoni mwa mwaka huu.
Waziri huyo alisema kuwa suala la mazingira linamhusu kila mtu hivyo kuna umuhimu wa kuwahusisha wadau kama wafanyabishara, sekta binafsi na taasisi za dini ambao watatoa mchango wa hali na mali katika kuchangia mfuko wa mazingira.
“Upo umuhimu kwa Ofisi ya Makamu wa Rais na NBS kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kupata takwimu sahihi za hali halisi ya mazingira ili kuweza kukabiliana nazo na ningependa kuona pia utafiti na takwimu zichukuliwe katika mikoa mingine ikiwemo Geita, Singida, Dodoma na Tabora ambayo inaathiriwa na ukataji miti,” alisema.
Aidha alisisitiza kuwa masuala ya mazingira yaelekezwe katika ngazi ya Serikali za Mitaa ambako kule ni rahisi kuwafikia wananchikwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.