Naibu Waziri wa Madini Stanislaus Nyongo,akitolea ufafnuzi tuhuma zilizotolewa kuhusiana na uchimbaji madini Mererani wakati kizungumza na washiriki kutoka Taasisi mbalimbali nchini katika mkutano wa majadiliano ya Wiki ya Azaki inayoendelea jijini Dodoma.
Mchimbaji mdogo wa madini ya Tanzanite kutoka jijini Arusha Bi.Kanaeli Minja,akimuuliza swali Naibu waziri wa madini Mhe.Stanislaus Nyongo (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na washiriki kutoka Taasisi mbalimbali nchini katika mkutano wa majadiliano ya Wiki ya Azaki inayoendelea jijini Dodoma.
Sehemun ya Viongozi na washiriki kutoka Taasisi mbalimbali nchini wakifatilia mkutano wa majadiliano ya Wiki ya Azaki inayoendelea jijini Dodoma.
…………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, amekanusha kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji katika mgodi wa madini ya Tanzanite uliopo Mererani mkoani Manyara.
Nyongo ametoa kauli hiyo leo katika Jukwaa la tisa la Asasi za Kiraia (AZAKI) ikiwa ni sehemu ya mijadala inayoendelea kwenye wiki ya AZAKI jijini Dodoma baada ya mchimbaji mdogo wa madini hayo kutoka jijini Arusha Kanaeli Minja kutoa malalamiko hayo.
Mchimbaji huyo ameeleza kuwa licha ya Serikali kutoa mwongozo wa kufungwa kwa mashine za ukaguzi,lakini hadi sasa mashine hizo hazijafungwa na wameendelea kudhalilika kwa kuachwa utupu hata kama wakionesha ushirikiano katika zoezi hilo la ukaguzi ili kuingia mgodini.
“Kuna vitendo vya udhalilishaji wanawake wanavuliwa nguo na kuachwa utupu mbele ya watoto wadogo hata wakionesha ushirikiano katika zoezi la ukaguzi,” amesema Mchimbaji huyo.
Kanaeli ameiomba serikali kukemea tabia hiyo pamoja sambamba na viongozi wanaosimamia mgodi huo kufunga mashine hizo ambazo zitarahisisha ukaguzi na kudhibiti utoroshwaji wa madini.
Aidha ameishauri serikali kutunga sheria kwa kuangalia wananchi wa chini na wabunge wasipitishe sheria kwa hati ya dharura kwa kuwa wananchi wa chini ndio wanaoathirika zaidi.
Akitoa ufafanuzi wa malalamiko hayo, Naibu Waziri Nyongo amesema kuwa sio kweli kuwa watu wananyanyaswa isipokuwa wengi wao hawataki kutoa ushirikiano wakati wa Ukaguzi.
“Kuna scanner zinazotumika kukagua madini ni maalum na ni za gharama kubwa, zina teknolojia kubwa tumeshaagiza.”
Amesisitiza “Si kweli kwamba watu wananyanyaswa baadhi yao hawataki kutoa ushirikiano wakati wa Ukaguzi,ndio maana maofisa wetu inabidi wawabane,kuhakikisha hakuna anayetoroka na madini hayo kwa namna yoyote ile’’amesema Nyongo.
Wiki ya AZAKI imezinduliwa Novemba 4 mwaka huu hivi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na itahitimishwa Novemba 8, Mwaka huu jijini Dodoma.