TANZANIA kupitia Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Masuala ya Haki za Ardhi la Landesa imepata fursa ya kuendesha Kampeni ya Haki Ardhi za Wanawake duniani ambayo itadumu kwa miaka 12.
Kampeni hiyo ambayo imeanza 2018 inatarajiwa kutekelezwa hadi 2030 kwa vipindi vya miaka mitatu mitatu.
Hayo yamesemwa na Mmoja wa Wakurugenzi wa Bodi ya Landesa Edna Sanga, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wameshiriki mafunzo ya siku mbili mjini Morogoro.
Alisema Tanzania imepata fursa ya kuzindua kampeni hiyo yenye kutaka wanawake wanamiliki ardhi kutokana na mchango wao kwa jamii.
Sanga alisema Landesa ambayo makao makuu yake nchini Marekani linaamini waandishi wa habari ni kiungo muhimu katika kutekeleza lengo hilo la kimataifa lenye kutaka mwanamke anamiliki ardhi kama walivyo wanaume kwa kuandika habari ambazo zitachochea kundi hilo kuonekana.
Alisema kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Novemba 21 mwaka huu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na. Watoto Ummy Mwalimu jambo ambalo litaamsha ari ya wanawake kutambua haki ya kumili ardhi kama chachu ya maendeleo.
“Landesa imeamua kuwashirikisha waandishi wa habari ili wawe washiriki wa kampeni hii, kwa miaka tisa tumekuwa tukizungumza umuhimu wa wanawake kumiliki ardhi ili waweze kuigeuza katika masuala ya kiuchumi hivyo wakati ndio huu kwa kushirikiana katika kampeni hii ya kidunia,” alisema.
Alisema utafiti uliofanywa unaonesha ni asilimia 24 ya wanawake ndio wanamiliki ardhi jambo ambalo linasikitisha kwani ulimwengu wa sasa unazungumzia uchumi na uchumi unahitaji ardhi ili shughuli za kiuchumi, kibiadhara na kijamii zinafanyika.
Alisema kampeni hiyo inapaswa kuwa ya kipekee ili iweze kuleta mabadiliko ya kiungozi na ubunifu hivyo amewataka waandishi wawe wabunifu kuitangaza kampeni hiyo muhimu ambayo imeanza kwa majaribio nchini.
Mkurugenzi huyo alisema Tanzania imepata nafasi hiyo kutokana na utashi wa kisiasa, sera, Sheria na ushirikiano uliopo katika kuinua mwanamke kwenye umilili ardhi.
Sanga alisema ujio wa kampeni hiyo ya Haki Ardhi za Mwanamke umechochewa na kuwepo kwa sera na sheria ila utekelezaji ulikuwa duni hivyo kampeni hiyo inayozinduliwa Novemba 21 itainua ari.