Home Mchanganyiko ZAIDI YA BILIONI MBILI KUTUMIKA KUSAMBAZA UMEME MAFIA

ZAIDI YA BILIONI MBILI KUTUMIKA KUSAMBAZA UMEME MAFIA

0

Wananchi wa kijiji cha chemchem wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati ambae hayupo pichani.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa kwanza kushoto) akimsikiliza Afisa wa Ardhi wa Wilaya ya Mafia, Chuchu Ochere Silvery (wa tatu kulia) ambae alikuwa anampa maelezo kuhusu eneo lilitolewa na wananchi wa Kanga kwa ujenzi wa mradi wa umeme wa upepo wa megawati tano.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, (wa nne kulia) akikata utepe kwenye nyumba ya Bi Rukia Muhammed Mbottoni (wa tatu kulia) katika kijiji cha Chemchem.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akiwasha umeme kwenye nyumba ya Bi Mtumwa Ally (hayupo pichani) katika kijiji cha Marimbani kata ya kiyegeani.

Costantine Koba ambaye ni Msimamizi wa Mitambo ya kufua umeme wilayani Mafia, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.

Naibu Waziri wa Nishati akiwasili kukagua mitambo ya kuzalisha umeme Wilaya ya Mafia.

************************************

Hafsa Omar – Mafia

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amesema kiasi cha shilingi bilioni mbili na milioni 800 zimetengwa kwa ajili ya kusambazia umeme wa jua kwa  visiwa vilivyopo wilayani Mafia, mkoani Pwani pamoja na vijiji vitatu ambavyo havijafikishiwa nishati hiyo.

Aliyasema hayo Novemba 4, mwaka huu katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Chemchem muda mfupi kabla ya kukiwashia umeme na kuongeza kwamba tayari maandalizi ya kutangaza tenda husika mwezi ujao yamekamilika.

Naibu Waziri alivitaja baadhi ya visiwa hivyo kuwa ni pamoja na Chole, Ibondo, Juani na Bwejuu. Alisema Serikali imedhamiria kupeleka umeme nchi nzima hata katika maeneo ambayo hayapitiki kwa urahisi.

“Wakati Rais anaingia madarakani aliahidi kusambaza umeme katika maeneo yote ambayo hayana umeme. Sisi Wizara tutahakikisha hilo linatekelezwa.”

Vilevile, aliwataka wananchi wa kijiji hicho kulinda miuondombinu ya umeme ili uweze kupatikana muda wote kwani sekta zote  muhimu za utalii na uvuvi zinategemea umeme wa uhakika. Aidha, aliwahimiza wananchi ambao miundombinu ya umeme imepita katika maeneo yao kulipia huduma hiyo ya umeme ili kujikwamua kiuchumi.

Naibu Waziri aliwatoa hofu wananchi ambao wameshalipa pesa kwa ajili ya kuunganishiwa umeme lakini mpaka sasa hawajaunganishwa na huduma hiyo, kuwa Serikali haitapokea  mradi ambao una mapungufu na kwamba kabla Mkandarasi hajakabidhi, mradi utakaguliwa.

“Nawataka wakandarasi wafanye kazi kwa mujibu wa mikataba.”

Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Rukia Muhammed Mbottoni aliishukuru Serikali kwa kuwapa unafuu wananchi wa vijijini kwa kuwaletea umeme wa REA ambao kila mwananchi anamudu gharama zake.

Alisema kuwa umeme wa REA umewawezesha kujiajiri kwa   kufanya biashara ndogondogo zinazowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Mbali na kijiji cha Chemchem, Naibu Waziri pia alikagua utekelezaji wa miradi ya nishati na kuwasha umeme katika kijiji cha Marimbani.

Aidha, alitembelea eneo ambalo litajengwa mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo na kukagua mitambo ya kufua umeme iliyopo  wilayani humo.